• HABARI MPYA

  Monday, June 11, 2018

  WACHEZAJI SIMBA SC WAFIKIA KWENYE USIKU WA TUZO ZA MO LEO...ZITAKUWA LIVE AZAM TV

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Simba SC kimerejea usiku wa kuamkia leo kutoka Kenya, ambako jana kilifungwa 2-0 na wenyeji, Gor Mahia katika fainali ya SportPesa Super Cup Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
  Mashujaa wa Gor Mahia jana walikuwa wanasoka wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere na Jaqcues Tuyisenge waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi na kurudia mafanikio ya mwaka jana mjini Dar es Salaam wakiwafunga mahasimu wao wa Kenya, AFC Leopard 3-0 na kutwaa taji hilo. 
  Kagere alianza kufunga bao zuri dakika ya sita akimalizia kazi nzuri ya George Odhiambo ‘Blackberry’ kabla ya Tuyisenge kufunga la pili akimalizia krosi ya Humphrey Mieno dakika ya 54.
  Kwa ushindi huo, Gor Mahia inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Muingereza Dylan Kerr pamoja na walizawadiwa dola za Kimarekani 30,000 lakini watakwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England.
   
  Simba SC wamejipatia dola za Kimarekani 10,000, Singida United waliomaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Kakamega Homeboyz kwa penalty 5-1 baada ya sare ya 1-1 watapatiwa dola 7, 500 na wa washindi wa nne watapewa dola 5,000.
  Kariobangi Sharks ya Kenya, Yanga ya Tanzania Bara na JKU ya Zanzibar kila moja itapata dola 2,500 baada ya kutolewa hatua ya kwanza ya mashindano. 
  Na leo wachezaji wa Simba wanatarajiwa kushiriki hafla ya tuzo za klabu hiyo zilizoandaliwa na Mwanahisa Mkuu mtarajiwa wa klabu, Mohammed Gulam Dewji kwa ajili ya wachezaji, viongozi na mashabiki zikijulikana kwa jina la Mo Simba Awards ambayo itafanyika katika hoteli ya Hyatt Regency – Kilimanjaro iliyopo mjini Dar es Salaam.
  Sherehe hiyo itakayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV itashuhudia vipengele 16 vya tuzo, ambavyo ni Mchezaji Bora wa Mwaka, Goli Bora la Mwaka, Golikipa Bora wa Mwaka, Beki Bora wa Mwaka, Kiungo Bora wa Mwaka, Mshambuliaji Bora wa Mwaka, Shabiki Bora wa Mwaka na Tuzo ya Heshima.
  Tuzo zingine ni Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka, Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Tuzo ya Benchi la Ufundi, Kiongozi Bora wa Mwaka, Tuzo ya Wasimamizi wa Mchakato wa Mabadiliko, Mhamasishaji Bora wa Mwaka katika Mitandao ya Kijamii, Mhamasishaji Bora wa Mwaka na Tawi Bora la Mwaka.
  Washindi wa tuzo hizo watatokana na kura ambazo zitapigwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya mosimbaawards.co.tz na kamati maalumu ya tuzo ambayo itahusisha wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
  Kwa mujibu wa Dewji, tuzo hizo kwa lengo la kutambua mchango wa wachezaji, viongozi na mashabiki ambao juhudi zao zimeiwezesha Simba SC kupata mafanikio iliyonayo sasa.
  Na Dewji pia anataka kutumia tuzo hizo kama sehemu ya mikakati yake ya kuifanya klabu ya Simba kuwa timu kubwa barani Afrika, ambayo itakuwa na uwezo wa kifedha ambao utaiwezesha kuwa na wachezaji na benchi la ufundi bora ambalo litaiwezesha kushinda mataji makubwa.
  Simba SC imemaliza vizuri msimu, ikitwaa mataji mawili, kwanza Ngao ya Jamii na baadaye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuelekea zama mpya za kumilikiwa na Mo Dewji, ameshinda zabuni ya kununua asilimia 49 ya hisa katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WACHEZAJI SIMBA SC WAFIKIA KWENYE USIKU WA TUZO ZA MO LEO...ZITAKUWA LIVE AZAM TV Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top