• HABARI MPYA

    Tuesday, June 05, 2018

    UNAWEZAJE KUZIPANGA KUNDI MOJA SIMBA NA YANGA KOMBE LA KAGAME? HATA EL MAAMRY, TENGA HAWAKUTHUBUTU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame Cup itafanyika tena baada ya miaka miwili ya kupotea kwake na kwa mara nyingine mwaka huu itaendeshwa nchini Tanzania kuanzia Juni 28 hadi Julai 13.
    Mechi zitachezwa katika viwanja viwili, Azam Complex uliopo Chamazi na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, huku mahasimu wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba SC na Yanga SC wakipangwa pamoja Kundi C.
    Akitaja makundi ya michuano hiyo mjini Dar es Salaam leo, Katibu wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye amesema kwamba pamoja na Simba na Yanga, timu nyingine katika Kundi hilo ni Dakadaha FC ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.
    Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) na Katibu wake, Wilfred Kidau (kushoto) wametoa mpya

    Musonye alisema kwamba Kundi A linaundwa na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na  Kator FC ya Sudan Kusini, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sport ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Djibouti.
    Musonye amesema kwamba wamelazimika kufanya mashindano ya mwaka huu sambamba na Fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi, kwa sababu wasipofanya mwezi huu hayatafanyika tena kwa mwaka wa tatu mfululizo. 
    Hata hivyo, Musonye amesema kwamba watatoa ratiba nzuri ambayo haitaruhusu mashindano ya mwaka huu kuingiliana na mechi za Kombe la Dunia.  
    Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Mhando alisema kwamba kwamba wataitumia michuano hiyo kukizindua kituo chao chao Redio, Uhai FM na akwahakikishia kwamba pamoja na mashindano hayo kufanyika sambamba na Kombe la Dunia, lakini yatafana 
    FIFA imeridhia Kagame kufanyika mwezi huu tofauti na agizo lake la kutotaka katika mwezi wa Fainali za Kombe la Dunia yasifanyike mashindano mengine yoyote, kwa sababu washiriki watano wa michuano hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, ambayo kwa sasa imesimama kupisha Kombe la Dunia itarejea Julai baada ya kumalizika kwa michuano hiyo nchini Urusi.
    Hao ni KCCA ya Uganda iliyopo Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye Kombe la Shirikisho ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda, Yanga ya Tanzania zilizopoi Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.

    Na kwa sababu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao msimu mpya wa Ligi Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika mwezi huu kuna hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
    Azam FC ndiyo mabingwa wa mwisho wa michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor Mahia 2-0 katika fainali Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya waliokuwa washambuliaji wake hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
    Na hiyo ndiyo ilikuwa michuano iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
    Baada ya kufungha mabao matano akiwa na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku , Osman Bilal Salaheldin wa Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na Tchetche wa Azam FC, Olunga akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016 iliyomuuza Guizhou Zhicheng mwaka 2017.
    Na Tanzania itawakilishwa na Azam FC kama mabingwa watetezi wa mashindano na Yanga SC, kama mabingwa wa nchi.
    Lakini mara baada ya kutoka kwa makundi na ratiba ya mashindano hayo, mjadala mkubwa umekuwa ni Yanga kupangwa kundi moja na SImba SC.
    Hizo ni kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla ambazo zinatarajiwa kuwa chachu ya mashindano na kuziweka pamoja ni kuharibu ladha ya mashindano.
    Kwa sababu kuna makundi matatu, ilipaswa kila timu mwenyeji ipewe kundi moja na baaada ya Azam FC kuwekwa Kundi A, ilitakiwa Simba na Yanga zigawanywe katika makundi B na C.
    Na hivyo ndivyo imekuwa miaka yote nah ii si mara ya kwanza wenyeji watatu kukutana katika mashindano hayo na hakuna mwaka ambao walipangwa pamoja katika hatua ya makundi.
    Mfano ni mwaka 2012 zote, Azam FC, Simba na Yanga ziliingia kwenye michuano hiyo lakini hazikuwekwa Kundi moja, labda kwa sababu wakati huo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alikuwa Leodegar Tenga, mtu wa mpira na mweledi. 
    Mwaka 2012 Kundi A lilikuwa linaundwa na Ports ya Djibouti, Simba, URA ya Uganda na waalikwa AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kundi lilikuwa na Azam FC, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya, wakati APR ya Rwanda, Atletico Olympic ya Burundi, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Yanga SC zilikuwa Kundi C.
    Hata Kenya hawawezi kuwa wenyeji wa Kombe la Kagame na wakaziweka pamoja timu zao katika makundi, vivyo kwa Uganda, Rwanda na Sudan.
    Haijulikani TFF chini ya Rais wake wa sasa, Wallace Karia wamefikiria nini kufanya hivyo kwa sababu hicho ni kitu kipya kabisa.
    Karia ametetea suala hilo katika mkutano akisema ni droo ilipangwa ikaziangushia timu hizo Kundi moja – bora kweli droo ingechezeshwa watu wakaona Yanga na Simba zinaangukia kundi moja, lakini huu ni utashi wa watu tu.
    Labda waaona Yanga sasa hivi wameyumba hawawezi kufika mbali katika mashindano bora wawakutanishe na Simba mapema wapate fedha nyingi kutokana na viingilio vya milangoni. Labda. Lakini kama hayo ndiyo mawazo ya watu waliopewa dhamana ya kuongoza soka ya nchi hii haitakuwa ajabu tukizidi kudidimia.
    Viongozi wote waliopita wa TFF kuanzia enzi za aki a Said El Maamry wakati wa FAT (Chama cha Soka Tanzania) hadi Leodegar Tenga hawakuwahi kufanya hivyo – ni uongozi wa sasa chini ya Rais Karia na Mtendaji wake Mkuu, Wilfred Kidau umethubutu. 
    Na hata kwa miaka yote ambayo Simba na Yanga zimekuwa zikikutana nje ya Tanzania kwenye michuano hii zimekuwa hazipangwi pamoja hatua ya makundi popote kwa sababu hata viongozi wa CECAFA wanajua kuhusu timu hizo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UNAWEZAJE KUZIPANGA KUNDI MOJA SIMBA NA YANGA KOMBE LA KAGAME? HATA EL MAAMRY, TENGA HAWAKUTHUBUTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top