• HABARI MPYA

  Saturday, June 09, 2018

  TEAM SAMATTA YAILAZA 4-2 TEAM KIBA, AJIBU AFUNGA MAWILI…BOBAN ANG’ARA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TIMU ya mwanasoka Mbwana Ally Samatta na Rafiki zake imefanikiwa kushinda mabao 4-2 dhidi ya mwanamuziki Ally ‘King’ Kiba na Marafiki zake katika mchezo maalum wa kirafiki wa Hisani uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa zamani wa kimataifa wa FIFA, Osman Kazi, Team Kiba ilitangulia kwa mabao ya mshambuliaji wa Yanga SC, Ibrahim Ajibu Migomba dakika za tatu na 30, kabla ya Team Samatta kuzinduka na kusawazisha yote ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
  Na mabao yote yalitokana juhudi za ndugu wa damu, watoto wa mzee Ally Samatta, Mohammed anayechezea Mbeya City na mdogo wake Mbwana wa KRC Genk ya Ubelgiji.
  Mbwana Samatta (kulia) akitafuta maarifa ya kumpita beki kizingiti wa Team Kiba, Mohammed Bin Slum (kushoto) 
  Ibrahim Ajibu wa Team Kiba (kulia) akipambana na Super Jamhuri Kihwelo (chini) wa Team Samatta 
  Haruna Moshi 'Boban' wa Team Samatta (kulia) akiambaa na mpira baada ya kuwatoka mabeki wa Team Samatta, Aggrey Morris na Mohammed Bin Slum  
  Thomas Ulimwengu wa Team Samatta akiwatoka viungo wa Team Kiba, Ally Kiba na Said Ndemla 

  Uhuru Suleiman wa Team Kiba akimiliki mpira mbele ya Mohammed Samatta wa Team Samatta

  Moudy Samatta alianza kufunga kwa shuti kali dakika ya 35 baada ya kazi nzuri ya Henry Joseph Shindika wa Mtibwa Sugar na dakika ya 40, Super Jamhuri anayecheza Qatar akaisawazishia Team Samatta kwa penalti baada ya Mbwana Samatta kuchezewa rafu kwenye boksi na Said Ndemla wa Simba. 
  Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko karibu ya wachezaji wote, Team Kiba ikiwa chini ya kocha Freddy Felix Minziro na Samatta chini ya kocha Jamhuri Kihwelo.
  Mabadiliko hayo yaliinufaisha Team Samatta ambayo ilivuna mabao mabao mawili zaidi na kuopata ushindi wake wa 4-2. 
  Alianza kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na Gefle IF ya Sweden, Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye kwa sasa anachezea Friends Rangers kuifungia Team Samatta bao la tatu dakika ya 50 kwa ustadi wa hali ya juu.
  Na Ally Kiba akapoteza nafasi ya kuisawazishia timu yake dakika ya 52, baada ya kupiga juu ya lango mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Kazi, baada ya beki wa Yanga, Nadi Haroub ‘Cannavaro’ kumchezea rafu winga Simon Msuva anayechezea Difaa Hassan El- Jadida ya Morocco.
  Na Samatta akaupendezesha ushindi wa timu yake kwa kufunga bao zuri la nne dakika ya 56 kabla ya kuondosha uwanjani akimpisha mshambuliaji, Rashid Yusuph Mandawa anayechezea BDF ya Botswana.
  Ulikuwa mchezo maalum wa hisani uliopewa jina #Nifuate ni wa kuhamasisha uchangiaji wa vifaa na miundombinu mashuleni, ambao fedha zilizopatikana kutokana na viingilio zitanunuliwa madawati na kusaidia ujenzi wa vyoo mashuleni. 
  Vikosi vilivyoanza; Team Samatta; Juma Kaseja, Hassan Kessy, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Henry Joseph, Haruna Moshi ‘Boban’/Athumani Iddi Chuji, Mbwana Samatta/Rashid Mandawa, Super Jamhuri/Amri Kiemba, Mohammed Samatta na Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngassa.  
  Team Kiba; Shaaban Kado, Mohammed Bin Slum, Stanley Nkomola, Abdi Banda, Aggrey Morris, Abdi Kassim, Uhuru Suleiman, Said Ndemla, Ali Kiba, Ibhrahim Ajib na Simon Msuva.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TEAM SAMATTA YAILAZA 4-2 TEAM KIBA, AJIBU AFUNGA MAWILI…BOBAN ANG’ARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top