• HABARI MPYA

    Thursday, June 07, 2018

    SIMBA SC WATIBUANA NA KOCHA WAO MFARANSA, AISUSA TIMU NAKURU AKAA JUKWAANI

    Na Mwandishi Wetu, NAKURU
    UGONJWA wa Simba SC kutodumu na makocha wake unaweza kuendelea baada ya kutofautiana na kocha wake, Mfaransa Pierre Lechantre aliyeanza kazi Januari 18 tu, mwaka huu.
    Lechantre na Msaidizi wake aliyekuja naye, Mtunisia Aymen Hbibi Mohammed leo walikuwa jukwaani wakati Simba SC ikimenyana Simba SC na Kakamega Homeboyz katika Nusu Fainali ya SportPesa Super Cup na kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Afraha pia.
    Timu iliongozwa na Kocha Msaidizi, Mrundi Masoud Juma aliyekaa benchi na kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ na jukwaani alikuwepo Kaimu Rais wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’.
    Pierre Lechantre (kushoto) na Msaidizi wake, Mtunisia Aymen Hbibi Mohammed walikuwa jukwaani leo.Tazam video chini↓



    Kocha Msaidizi, Masoud Juma (kulia) aliiongoza timu kwa kushirikiana na kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ (wa pili kutoka kulia) 

    Dalili za Simba SC kutodumu na kocha huyo zilianza kuonekana mapema tu baada ya Lechantre kuomba kazi ya kuifundisha timu ya taifa ya Cameroon Aprili mwaka huu.
    Na baada ya Ligi Kuu kumalizika, Simba SC ikitwaa ubingwa wa kwanza tangu mwaka 2012, iliibuka minong’ono Simba SC haiweze kuendelea na Mfaransa huyo kwa sababu ya mshahara mkubwa.
    Lakini pia minong’ono mingine ilikuwa inasema kwamba  viongozi wa Simba hawapendezewi tabia ya ukali wa kupitiliza wa kocha huyo kiasi cha kutopenda hata kuzungumza wala kupokea ushauri.
    Na taarifa zilisema asingekuwepo hata kwenye msafara wa timu Kenya kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, lakini ikawa toafuti amekwenda ingawa sasa mambo yamekuwa makubwa. 
    Haitakuwa ajabu wakati wowote uongozi wa Simba SC ukitangaza rasmi kuachana na Mfaransa huyo ambaye mkataba wake wa miezi sita unafikia tamati mwezi huu.
    Lechantre alichukua nafasi ya Mcameroon Joseph Marius Omog na ameiongoza timu katika mechi 22 tu, ukiondoa mchezo wa leo ambao alikuwa jukwaani, ikishinda 14, sare saba na kufungwa moja.
    Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018 itafanyika Jumapili na mshindi pamoja na kupata dola za Kimarekani 30,000 pia atapata nafasi ya kwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England. 
    Mshindi wa pili atajipatia dola za Kimarekani 10,000, wa tatu dola 7, 500 na wa nne dola 5,000 wakati timu nyingine zitapewa kifuta jasho cha dola 2,500. 
    Bingwa mtetezi ni Gor Mahia ambayo mwaka jana iliifunga AFC Leopards 2-1 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WATIBUANA NA KOCHA WAO MFARANSA, AISUSA TIMU NAKURU AKAA JUKWAANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top