• HABARI MPYA

    Tuesday, June 05, 2018

    SIMBA NA YANGA KUMENYANA JULAI 5 KOMBE LA KAGAME UWANJA WA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    VIGOGO wa soka Tanzania, Simba SC na Yanga SC zitamenyana Julai 5, mwaka huu katika mechi ya Kundi C michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame Cup inayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
    Akitaja makundi ya michuano hiyo, Katibu wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema kwamba pamoja na Simba na Yanga, timu nyingine katika Kundi hilo ni Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.
    Musonye alisema kwamba Kundi A linaundwa na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator FC wa Sudan Kusini, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sport ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Djibouti.

    Musonye aliishukuru Tanzania kwa kukubali kuwa wenyeji wa michuano hiyo na akasema kwamba anatarajia itafana kwa sababu ya rekodi ya nchi hii kuandaa mashindano yalioykuwa na msisimko mkubwa miaka ya nyuma.
    Musonye ambaye alisema mashindano yatafanyika viwanja vya Taifa na Azam Complex, Chamazi – pia amewapongeza Rwanda na Rais wao, Paul Kagame kwa kuwa wadhamini wa mashindano haya kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
    Musonye amesema kwamba wamelazimika kufanya mashindano ya mwaka huu sambamba na Fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi, kwa sababu wasipofanya mwezi huu hayatafanyika tena kwa mwaka wa tatu mfululizo. 
    Hata hivyo, Musonye amesema kwamba watatoa ratiba nzuri ambayo haitaruhusu mashindano ya mwaka huu kuingiliana na mechi za Kombe la Dunia.  
    Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Mhando alisema kwamba kwamba wataitumia michuano hiyo kukizindua kituo chao chao Redio, Uhai FM na akwahakikishia kwamba pamoja na mashindano hayo kufanyika sambamba na Kombe la Dunia, lakini yatafana 
    FIFA imeridhia Kagame kufanyika mwezi huu tofauti na agizo lake la kutotaka katika mwezi wa Fainali za Kombe la Dunia yasifanyike mashindano mengine yoyote, kwa sababu washiriki watano wa michuano hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, ambayo kwa sasa imesimama kupisha Kombe la Dunia itarejea Julai baada ya kumalizika kwa michuano hiyo nchini Urusi.
    Hao ni KCCA ya Uganda iliyopo Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye Kombe la Shirikisho ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda, Yanga ya Tanzania zilizopoi Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.
    Na kwa sababu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao msimu mpya wa Ligi Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika mwezi huu kuna hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
    Azam FC ndiyo mabingwa wa mwisho wa michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor Mahia 2-0 katika fainali Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya waliokuwa washambuliaji wake hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
    Na hiyo ndiyo ilikuwa michuano iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
    Baada ya kufungha mabao matano akiwa na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku , Osman Bilal Salaheldin wa Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na Tchetche wa Azam FC, Olunga akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016 iliyomuuza Guizhou Zhicheng mwaka 2017.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA KUMENYANA JULAI 5 KOMBE LA KAGAME UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top