• HABARI MPYA

    Thursday, June 07, 2018

    SALAMBA TAYARI YUPO NAKURU KUIONGEZEA NGUVU SIMBA IKIMENYANA NA KAKAMEGA LEO

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Adam Salamba aliyesajiliwa kutoka Lipuli ya Iringa mwezi uliopita amewasili nchini Kenya kwa ajili ya kuiongezea nguvu timu hiyo kwenye michuano ya SportSpesa Super Cup inayoendelea mjinu Nakuru.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online jana, Kocha Msaidizi wa Klabu ya Simba, Masoud Juma amesema kwamba kwa ukubwa wa mashindano haya na kwa kuwa Salamba tayari ni mchezaji halali wa klabu hiyo wameona ni vyema aje aongeze nguvu katika kikosi cha timu hiyo ambacho leo kinashuka dimbani kumenyana na Kakamega kwenye mchezo wa Nusu Fainali ya mashindano hayo.

    Adam Salamba amewasili Nakuru kuiongezea nguvu Simba SC michuano ya SportSpesa Super Cup  

    "Ni kweli Adam Salamba amekwishafika nchini Kenya kwa ajili ya kuongeza nguvu katika Kikosi chetu kwa sababu tayari ni mchezaji halali wa klabu yetu, hivyo tumeona ni vizuri aje kutia nguvu katika mashindano haya ya SportSpesa Super Cup,"amesema Masoud Juma
    Juma ameongeza kuwa kwa mchezo wa leo ambao ni Nusu Fainali ya mashindano hayo utakuwa ni muhimu sana kwao kushinda waingie Fainali. 
    Nusu Fainali za SportPesa Super Cup zinafanyika leo Uwanja wa Afraha mjini Nakuru zikikutanisha timu za Tanzania na wenyeji, Kenya. 
    Simba SC watamenyana na Kakamega Homeboyz wakati Singida United watamenyana na Gor Mahia ya Kenya.
    Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018 itafanyika Jumapili na mshindi pamoja na kupata dola za Kimarekani 30,000 pia atapata nafasi ya kwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England. 
    Mshindi wa pili atajipatia dola za Kimarekani 10,000, wa tatu dola 7, 500 na wa nne dola 5,000 wakati timu nyingine zitapewa kifuta jasho cha dola 2,500. 
    Bingwa mtetezi ni Gor Mahia ambayo mwaka jana iliifunga AFC Leopards 2-1 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SALAMBA TAYARI YUPO NAKURU KUIONGEZEA NGUVU SIMBA IKIMENYANA NA KAKAMEGA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top