• HABARI MPYA

  Friday, June 08, 2018

  NGOMA NJE MIEZI MIWILI NA NUSU ZAIDI, AZAM FC KUMSAJILI NCHIMBI WA NJOMBE MJI FC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mzimbabwe, Donald Ngoma atakuwa nje kwa miezi miwili na nusu baada ya kujiunga na Azam FC akiendelea na matibabu ya mguu wake alioumia akiwa Yanga.
  Hiyo ni baada ya vipimo alivyofanyiwa nchini Afrika Kusini wiki iliyopita na kupewa matibabu na programu maalum ya mazoezi, ambavyo ataendelea navyo kwa miezi miwili na nusu kabla ya kurudi rasmi uwanjani.
  Azam FC ilimchukua Ngoma kwa makubaliano ya akafanyiwe vipimo ambayo vikiwa na majibu mazuri atapewa mkataba. Na habari zinasema baada ya vipimo hivyo nchini Afrika Kusini ambako aliongozana na Daktari Mkuu wa klabu, Mwanandi Mwankemwa, Azam FC imeridhika kumsajili Ngoma.
  Donald Ngoma atakuwa nje kwa miezi miwili na nusu baada ya kujiunga na Azam FC 

  Beki chipukizi wa kulia Azam FC, Abdul Omary ‘Hamahama’, ameongezewa mkataba wa miaka miwili 

  Ngoma na Mwankemwa wanatarajiwa kurejea mjini Dar es Salaam leo usiku na kesho atasaini mkataba wa kujiunga rasmi na Azam FC.
  Baada ya kusaini, Ngoma atakwenda kwao Zimbabwe kwa mapumziko ya wiki tatu kabla ya kurejea Dar es Salaam kuanza rasmi kazi. 
  Wakati huo huo: Azam FC inataka kumsajili mshambuliaji Ditram Nchimbi kutoka Njombe Mji FC iliyoshuka Daraja, ambaye akisaini atakuwa mchezaji mpya wa tatu Azam FC baada ya Ngoma na Mzimbabwe mwingine, kiungo Tafadzwa Kutinyu – ambao wote mikataba yao ni ya mwaka mmoja.
  Katika hatua nyingine, beki chipukizi wa kulia Azam FC, Abdul Omary ‘Hamahama’, ameongezewa mkataba wa miaka miwili zaidi kuendelea kuitumikia timu hiyo.
  Hamahama mwenye umri wa miaka 19, ni zao la Azam Academy akilelewa tangu wakati kikosi hicho kikifundishwa na Vivek Nagul raia India, ambapo alipandishwa rasmi timu kubwa msimu ulioisha 2017/2018 na kufanikiwa kucheza mechi nne za mwisho za Azam FC kwa kiwango cha juu.
  Wakati akipandishwa alipewa mkataba wa miaka miwili, na mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) alizocheza ni ile Azam FC iliyopoteza ugenini dhidi ya Stand United (2-1), nyingine ikizifunga Majimaji (2-0), Tanzania Prisons (4-1) na Yanga (3-1).
  Zoezi la beki huyo kuingia mkabata mpya limesimamiwa na Meneja wa timu, Phillip Alando, ambaye wakati akiwa Meneja wa timu ndogo alishiriki kung’amua kipaji cha Hamahama, akimpendekeza kwa Kocha Nagul kabla ya kusajiliwa.
  Aidha kwa kusaini mkataba huo mpya, beki huyo mfupi, mwenye spidi na uwezo wa kupiga krosi nzuri zenye madhara, kutamfanya kuendelea kuitumikia Azam FC hadi mwaka 2021.
  Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB inayoongoza kwa ubora na usalama wa fedha zako nchini, maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, imejipambanua kwa kuwekeza vilivyo kwenye soka la vijana ikiwa na vikosi kuanzia umri chini ya miaka 11 hadi 20 (U-11 hadi U-20).
  Kila msimu imekuwa na utaratibu wa kupandisha timu kubwa vijana wanaofanya vizuri, msimu uliopita ikiwatumia wanne akiwemo Hamahama, wengine wakiwa ni washambuliaji Yahya Zaid, Paul Peter na beki wa kati Oscar Masai.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGOMA NJE MIEZI MIWILI NA NUSU ZAIDI, AZAM FC KUMSAJILI NCHIMBI WA NJOMBE MJI FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top