• HABARI MPYA

  Friday, June 01, 2018

  NDAYIRAGIJJE ‘AWAACHIA VUMBI’ SINGIDA UNITED, ATUA MANISPAA YA KINONDONI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mrundi, Ettiene Ndayiragijje leo amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuifundisha timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) iliyopanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao. 
  Ndayiragijje anajiunga na KMC akitokea klabu ya Mbao FC ya Mwanza ambako amedumu kwa misimu miwili tangu ajiunge nao akitokea kwao Burundi.
  Na kutua kwa Ndayiragijje KMC, kunazima tetesi kwamba Mrundi huyo alikuwa mbioni kujiunga na Singida United ambayo kesho itaagana na kocha wake, Mholanzi, Hans van der Pluijm anayehamia Azam FC.
  Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta (kushoto) akibadilishana mikataba na Kocha Mrundi, Ettiene Ndayiragijje leo mjini Dar es Salaam

  Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta (kushoto) akitiliana saini mikataba na Kocha Mrundi, Ettiene Ndayiragijje leo mjini Dar es Salaam

  Ndayiragijje ametia saini ya kujiunga na KMC leo asubuhi kwenye ofisi za Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta mjini Dar es Salaam.
  Na baada ya kusaini mkataba huo, Sitta amesema kwamba wao kama Bodi ya timu hiyo, wameamua kumchukua kocha huyo kwa sababu wanaamimi atawasaidia kutimiza malengo yao.
  “Sisi tunataka si tu kucheza Ligi Kuu kwa mafanikio, bali pia tutaanzisha chuo cha vipaji vya soka (Academy) kwa vijana wadogo na tumeona mwalimu huyu atatufaa. Na kwa sababu hii ni timu ya wananchi wa Kinondoni, tunatarajiwa ataibua vipaji vingi,”amesema Sitta.
  Kwa upande wake, Ndayiragijje alisema kwamba anashukuru kujiunga na timu hiyo na anatarajia kwa ushirikiano mkubwa atakaopewa anaweza kujenga timu bora.
  Ndayiragijje amejipatia umaarufu mkubwa katika misimu miwili ya kuwa na Mbao FC, akiifanya kuwa timu tishio katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara – na pia msimu uliopita aliifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kanla ya kufungwa 2-1 na Simba SC waliokuwa mabingwa.
  Lakini katikati ya msimu huu Mrundi huyo alitofautiana na uongozi wa Mbao FC na akaachana na timu baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDAYIRAGIJJE ‘AWAACHIA VUMBI’ SINGIDA UNITED, ATUA MANISPAA YA KINONDONI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top