• HABARI MPYA

    Tuesday, June 12, 2018

    MWAMEJA, MASATU WALIFIKIRIWA KWENYE TUZO YA MAFANIKIO YA MUDA WOTE?

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SHUGHULI ya tuzo za wachezaji Simba SC imefana jana katika hoteli ya kifahari, Hyatt Regency – The Kilimanjaro Nahodha na mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa klabu.
    Bocco alitwaa tuzo hiyo akiwaangusha wachezaji wenzake, winga Shiza Ramadhani Kichuya na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi na akabeba tuzo nyingine, ya Bao Bora la Msimu, alilofunga dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.
    Lakini Kichuya na Okwi nao hawakuondoka watupu, kwani mshambuliaji kutoka Uganda alibeba tuzo ya mshambuliaji bora na winga wa kimataifa wa Tanzania akabeba tuzo ya Kiungo Bora. Katika tuzo ya kiungo Bora, Kichuya aliwaangusha Jonas Mkude na Mghana, James Kotei. Okwi naye akawashinda Kichuya na Bocco kuwa mshambuliaji bora.

    Mwameja Mohammed akikiongoza kikosi cha Simba SC katika moja ya mechi zake mwaka 1993. Anayemfuatia ni George Masatu

    Aishi Manula akawaangusha Said Mohamed 'Nduda' na Emmanuel Elias Mseja kuwa kipa bora, Erasto Nyoni akawashinda Yusuph Mlipili na Shomari Kapombe kuwa beki bora, Zainab Rashid Pazi akawashinda Rukia Salum na Dotto Makunja kuwa Mchezaji Bora wa Kike. 
    Rashid Juma akawashinda Salum Shaaban na Ally Salim kuwa Mchezaji Bora Chipukizi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi akamkabidhi tuzo ya Heshima kwa Mafanikio ya Muda Wote, kiungo na kocha wa zamani wa klabu, Suleiman Abdallah Matola.
    Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ akatunukiwa tuzo ya Kiongozi Bora wa Msimu, marehemu Fihi Salehe Kambi akatunikiwa tuzo ya Shabiki Bora wa Msimu, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ akawashinda Salama Jabir, Mbunge Zitto Kabwe, mwigizaji Vyonne Cherrie ‘Monalisa’ na mwimbaji mwenzake, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ kushinda tuzo ya Mhamasishaji Bora kwenye Mitandao.
    Msemaji wa timu, Haji Manara akashinda tuzo ya Mhamasishaji Bora wa Jumla akimuangusha Mzee Muchacho, shabiki wa miaka mingi wa Simba SC na Ubungo Terminal likashinda tuzo ya Tawi Bora la Msimu likiyashinda matawi ya Wazo Hill na Vuvuzela.
    Kukatolewa tuzo maalum za benchi la Ufundi zilizokwenda kwa Kocha Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre, Msaidizi wake, Mrundi, Masoud Djuma, Kocha wa Mazoezi ya Viungo Mtunisia Aymen Mohamed Hbibi, kocha wa makipa Muharami Mohamed ‘Shilton’, Meneja Richard Robert, Daktari Yassin Gembe na Mratibu Abbas Selemani.
    Ikatolewa pia tuzo ya Wasimamizi wa mchakato wa mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu kuingia kwenye soko la Hisa, ambayo walikabidhiwa Jaji Mstaafu Thomasi Mihayo, Wakili Damasi Ndumbaro, Abdulrazak Badru, Mussa Hassan Zungu, Yusuph Nassoro, Brenda Mrema na Mzee Hamis Boma.
    Wengine ni Revocatus Cosmas Sangu, Hashim Nyendage, Gervas Alpha Honest, Emmanuel Metusela Urembo, Mulamu Nghambi, Suleiman Omari, Aziz Kifile, Salim Abdallah Muhene, Arnold Kashembe, Omari Bakari Mtika na Evodius Mtawala.
    Tuzo hizo zilihudhuriwa na Rais Mstaafu Mwinyi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na mwanamuziki nyota, Nassib Abdul ‘Diamond’ aliyemkabidhi tuzo rafiki yake, Hajji Manara. Ikumbukwe, Simba imemaliza msimu vizuri kwa mataji mawili, Ngao ya Jamii na ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. 
    Maswali yalianza kuibuka juu ya tuzo hizo wakati tu wa kutaja vipengele, ziko tofauti mno na tuzo nyingine za klabu zilizozoeleka kote duniani – hizi za Mo Simba zinazidi hata zile za mashindano, Ligi tuzo za nchi za Mwaka.
    Lakini kwa kuwa ni mtu ameamua kuanzisha kitu chake, kwa utashi wake na ameshirikisha watu kama ilivyoelezwa jana, kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Waandishi wa Habari waliobobea huwezi kumuingilia zaidi ya kusubiri kuona.
    Na jana tumeona. Tuzo zimefana, kipa bora wazi ni kipa namba moja, Aishi Manula, beki bora Erasto Nyoni safi kabisa amekuwa na msimu mzuri kuliko mchezaji mwingine yeyote wa safu ya ushambuliaji – Kichuya kiungo bora huwezi kuikataa pia, Okwi mshambuliaji bora ni sahihi na hata Bao Bora la Bocco sadakta.
    Sehemu ambayo watu wamebaki wanajiuliza ni kwenye Tuzo ya Mafanikio ya Muda Wote ambayo ilichukuliwa na Suleiman Matola Nahodha, kiungo wa zamani wa klabu na aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi pia. 
    Kwanza ni mapema sana Matola kuanza kufikiriwa kwenye tuzo za aina hiyo sababu rekodi zinaonyesha hadi mwaka 2010 alikuwa anacheza soka ya ushindani. Real Madrid wenyewe hawajaanza kumfikiria Ronaldo Lima kwenye tuzo ya mafanikio ya muda mrefu. 
    Inawezekana Simba SC wamechoka kuendelea kumpa heshima hiyo Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King’ Kibadeni na sasa wanataka wapewe na wachezaji wengine pia – lakini je kwa sasa ni sahihi kumpa Matola mbele ya magwiji wengine wa Simba waliocheza baada ya Kibadeni, miaka ya 1980 na 1990?
    Au Kamati ya Tuzo iliundwa na watu wachanga ambao wameanza kuijua Simba SC miaka ya 2000 wakaona Matola ni mtu sahihi kwa tuzo hiyo? 
    Kuna watu wamefanya makubwa pale Simba SC na wamecheza kwa muda mrefu kama Mwameja Mohammed ambaye alicheza kuanzia mwaka 1992 hadi 2002, ukiondoa miaka miwili aliyokwenda Reading ya England kati ya 1996 na 1997 kabla ya kurejea mwaka 1998 na akasajiliwa kwa msimu wa 1999.
    Mwameja ni mshindi wa mataji matatu ya Klabu Bingwa Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame katika miaka ya 1992, 1995 na 2002 na aliyeifikisha timu katika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993– achilia mbali mataji ya Ligi Kuu, Ligi ya Muungano, Kombe la Chama cha Soka Tanzania (FAT) na Kombe la Nyerere. 
    Huyo ni mmoja tu na sitaki kurudi zama za akina Kibadeni na wenzake Athumani Mambosasa, Athumani Juma Kalomba, Khalid Abeid, Haidari Abeid walioifikisha Simba Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika – au enzi za akina Zamoyoni Mogella, ‘Super’ Kihwelo Mussa, Nico Njohole miaka ya 1980, lakini kuna George Magere Masatu, beki kisiki wa muda mrefu miaka ya 1990 Msimbazi na mshindi wa mataji mengi, ikiwemo fainali ya CAF.  Wote walifikiriwa katika tuzo hiyo?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAMEJA, MASATU WALIFIKIRIWA KWENYE TUZO YA MAFANIKIO YA MUDA WOTE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top