• HABARI MPYA

    Sunday, June 10, 2018

    MAWAZIRI MWAKYEMBE, MKUCHIKA WAWAWEKA ‘KITI MOTO’ VIONGOZI YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison George Mwakyembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Huruma Mkuchika wamekaa faragha na uongozi wa Yanga kabla ya kuanza kwa mkutano Mkuu wa klabu hiyo Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
    Mawaziri hao waliketi na uongozi huo, chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga katika chumba cha maalum ch mikutano kwenye ukumbi huo kwa takriban nusu saa.
    Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya, Jaji John Mkwawa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa.
    Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika (kushoto) na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clemernt Sanga katika kikao hicho
    Kushoto kwa Waziri Mwakyembe, Waziri Mkuchika na  Sanga ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika
    Mawaziri wa Mwakyembe na Mkuchika katika kikao na viongozi wa Yanga
    Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya, Jaji John Mkwawa (katikati)
    Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa aliyesimama

    Na baada ya hapo wakatoka kuingia kwenye mkutano huo, ambao unatarajiwa kuwa suluhisho la matatizo ya Yanga yaliyodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja, tangu kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji Mei mwaka jana na klabu kuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga tangu hapo.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Kwa sasa klabu inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi kiasi cha kuambulia ushindi wa mechi moja kati ya 14 zilizopita, nyingine saba wakifungwa na sita kutoa sare. Na wana Yanga wako tayari Manji arejee kwa sharti lolote kuinusuru klabu.  Je, mkutano wa leo utakuwa mwanzo wa furaha tena kwa wana Yanga? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAWAZIRI MWAKYEMBE, MKUCHIKA WAWAWEKA ‘KITI MOTO’ VIONGOZI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top