• HABARI MPYA

    Wednesday, June 06, 2018

    MANYIKA MDOGO AJIZOLEA SIFA KIBAO KUOKOA PENALTI MBILI JANA KENYA

    Na Mwandishi Wetu, NAKURU
    MLINDA mlango Peter Manyika Junior amejizolea sifa kemkem kwa kuokoa penalty mbili jana na kuisaidia Singida United kwenda Nusu Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup.
    Singida United imeungana na Simba SC kwenda Nusu Fainali ya michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya pili, baada ya ushindi wa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 na AFC Leopards jana Uwanja wa Afraha, Nakuru nchini Kenya.
    Shujaa wa Singida United jana alikuwa kipa wake, Manyika Junior aliyeokoa penalti mbili, moja wakati wa dakika 90 za mchezo na nyingine kwenye mikwaju ya kuamua mshindi baada ya sare hiyo ya 0-0.
    Na kwa ujumla, Manyika aliyerithi kipaji cha baba yake, Manyika Peter mkubwa aliyekuwa kipa wa Yanga na timu ya taifa miaka ya 1990 mwishoni hadi 2000 mwanzoni, alikuwa nyota wa mchezo wa leo baada ya kuokoa michomo mingi ya hatari kwenye mchezo huo.

    Peter Manyika Junior alikuwa shujaa wa Singida United jana baada ya kuokoa penalti mbili na kuipeleka Nusu Fainali SportPesa SuperCup

    Na baada ya mchezo, Manyika amejizolea pongezi kedekede kutoka kwa wadau wa soka, wakiwemo viongozi na wachezaji wenzake.
    Miongoni mwao ni Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jemadari Said ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika; “Hongera kipa! Inaonekana nyie makipa wa Tanzania mmeamua kuonyesha ubora wetu kwenye penalty,”.
    Msemaji wa klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara amemsifu Manyika pia katika ukurasa wake Instagram akisema; Wa kuitwa Junior Manyika umetisha sana mwana,”. Manara akaenda mbali zaidi kwa kuandika; “Kama wao waliingia fainali mwaka jana kwetu…kwa nini mwaka huu tusiingie Simba na Singida United fainali ya SportPesa Super Cup huku kenya?,”
    Kwa ushindi wa jana, Singida United imelipa kisasi cha kutolewa na A.F.C. Leopards kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 mwaka jana mjini Dar es Salaam katika hatua kama hii michuano hiyo ikifanyika kwa mara ya kwanza.
    Singida United ikicheza kwa mara ya kwanza chini ya kocha mpya, Hemed Morocco leo, sasa itakutana na Gor Mahia katika Nusu Fainali, wakati Simba SC iliyoitoa Kariobangi kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 0-0 itamenyana na Kakamega Homeboyz Juni 7.      
    Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018 itafanyika Juni 10 na mshindi pamoja na kupata dola za Kimarekani 30,000 pia atapata nafasi ya kwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England. 
    Mshindi wa pili atajipatia dola za Kimarekani 10,000, wa tatu dola 7, 500 na wa nne dola 5,000 wakati timu nyingine zitapewa kifuta jasho cha dola 2,500. 
    Bingwa mtetezi ni Gor Mahia ambayo mwaka jana iliifunga AFC Leopards 2-1 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANYIKA MDOGO AJIZOLEA SIFA KIBAO KUOKOA PENALTI MBILI JANA KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top