• HABARI MPYA

  Tuesday, June 12, 2018

  MANYIKA ATAKA KUVUNJA MKATABA NA SINGIDA UNITED ADAI HAWAJAMLIPA STAHIKI ZAKE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MLINDA mlango Peter Manyika anafanya taratibu za kuvunja mkataba na klabu yake, Singida United kwa madai ya kutotekelezewa yaliyomo kwenye mkataba.
  Hayo yamesemwa na Meneja na baba wa mchezaji huyo, kipa wa zamani wa kimataifa nchini, Manyika Peter katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam.
  Manyika amesema kwamba Singida United wamekiuka vipengele vya mkataba na mwanawe, hivyo hawezi kurudi tena kuchezea timu hiyo, labda mambo yawekwe sawa.
  “Kuna malipo tulikubaliana wafanye, lakini hawajalipa na muda tuliokubaliana umepita, na pia mawasiliano yamekuwa magumu. Sasa huyu harudi tena kule, atabaki kituoni kwangu anafanya mazoezi,”amesema Manyika na kuongeza;
  “Alipokuwa Simba SC pia alikaa miaka mitatu bila kucheza, lakini akaja kituoni akafanya mazoezi akawa fiti Singida United wakamuona. Niko radhi akae mwaka mzima bila kucheza, lakini atafanya mazoezi kituoni na atarudi kazini baadaye,”.

  Peter Manyika anataka kuvunja mkataba na Singida United kwa madai hawajamlipa stahiki zake 

  Manyika amesema kwamba kutokana na usumbufu waliouonyesha Singida United ili mwanawe arudi huko pamoja na kumalizia deni, lakini pia lazima watoe ni mishahara ya mbele.
  Manyika alijiunga na Singida United Julai mwaka jana kwa mkataba wa miaka miwili, baada ya kuachana na Simba SC alikodumu kwa miaka mitatu kama kipa wa akiba.   
  Lakini alipoulizwa Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo pamoja na kukiri kipa huyo anadai sehemu ya fedha zake za usajili, alisema kwamba hajatafutwa na Manyika au baba yake juu ya madai hayo.
  “Ni taarifa ngeni, sijaona simu yoyote ya Manyika au baba yake. Na hata Manyika mwenyewe tulikuwa naye muda mwingi, tangu wakati hajaenda Kenya (kwenye michuano ya SportPesa Super Cup), lakini hajanikumbusha juu ya fedha zake,”. 
  Sanga Festo amesema kwamba inawezekana Manyika amepata ofa nzuri sehemu nyingine, sasa anataka kujaribu kuzua mtafaruku ili aondoke.
  “Ni kweli anatudai kwa maana ya fedha za usajili, lakini kwa mishahara hapana, hatudai. Makubaliano yalikuwa ni awamu mbili, bado awamu moja na hawajawahi kukumbusha,”amesema Sanga.
  Wiki iliyopita Manyika aling’ara kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, akiisaidia Singida United kumaliza katika nafasi ya tatu baada ya ushindi wa penalti 4-1 kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya wenyeji, Kakamega Homeboyz Uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Kenya.
  Manyika aliokoa penalti katika hatua ya Robo Fainali dhidi ya AFC Leopard ya Kenya pia na mechi ya kusaka mshindi wa tatu na kujizolea sifa nyingi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANYIKA ATAKA KUVUNJA MKATABA NA SINGIDA UNITED ADAI HAWAJAMLIPA STAHIKI ZAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top