• HABARI MPYA

  Wednesday, June 06, 2018

  MANARA ATABIRI SIMBA NA SINGIDA UNITED KUKUTANA FAINALI SPORTPESA SUPER CUP

  Na Mwandishi Wetu, NAKURU
  MSEMAJI wa klabu ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema kwamba inawezekana timu za Tanzania zikakutana kwenye Fainali ya SportPesa Super Cup Jumapili nchini Kenya.
  Singida United na Simba SC za Tanzania kesho zinaingia kwenye Nusu Fainali ya SportPesa Super Cup Uwanja wa Afraha mjini Nakuru nchini Kenya dhidi ya wenyeji na Manara amesema kwamba inawezekana wakazitoa Kakamega Homeboys na Gor Mahia na kwenda Fainali. 
  “Kama wao waliingia fainali mwaka jana kwetu…kwa nini mwaka huu tusiingie Simba na Singida United fainali ya SportPesa Super Cup huku Kenya?,”amesema Manara.
  Gor Mahia walikuwa mabingwa wa SportPesa Super Cup ya kwanza mwaka jana mjini Dar es Salaam wakiwafunga ndugu zao, AFC Leopards 2-1 katika mechi ya mahasimu mashemeji, maarufu kama ‘Derby ya Mashemeji’.
  Na kuelekea mechi za kesho za Nusu Fainali, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Juma amesema kwamba wataingia kwa nguvu tofauti na ilivyokuwa katika mechi yao ya kwanza wakishinda kwa penalti 3-2 dhidi ya Kariobangi Sharks baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90. 
  “Tulicheza vibaya (dhidi ya Kariobangi Sharks), kila mmoja wetu ameliona hilo. Hatuwezi kurejea tena kwa akili hiyo. Wachezaji wote wameona tunahitaji kubadilika kwenye mechi ya mwisho," alisema Juma.
  Naye Nahodha wa Simba SC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amesema; “Penalti siyo nzuri, ni kama bahati nasibu. Tulikuwa na mpango wa kushinda ndani ya dakika 90 tukashindwa dhidi ya Sharks lakini tutarejea tukiwa tofauti ili tuweze kushinda,".
  Kwa upande wake, kocha wa Singida United, Hemed Morocco amesema kwamba mechi na Gor Mahia itakuwa ngumu, lakini wataingia na mipango mipya ili washinde.
  “Itakuwa ni mechi ya tofauti sana na tuliyocheza na AFC Leopards, tutabadilika ili tuweze kushindana vizuri," alisema Morocco.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MANARA ATABIRI SIMBA NA SINGIDA UNITED KUKUTANA FAINALI SPORTPESA SUPER CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top