• HABARI MPYA

    Sunday, June 10, 2018

    KWA SASA KOMBE LA KAGAME HALINA FAIDA KWA YANGA, ZIFIKIRIWE SIMBA NA MTIBWA

    JUNI 5, mwaka huu Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetangaza rasmi kurejea kwa michuano ya Klabu Bingwa ukanda huu, maarufu kama Kombe la Kagame ambayo itaanza Juni 28 hadi Julai 13 ikifanyika katika viwanja viwili kwenye Jiji la Dar es Salaam, Taifa na Azam Complex, Chamazi vyote vipo Manispaa ya Temeke.
    Akitaja makundi ya michuano hiyo, Katibu wa kudumu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema vigogo wa Tanzania Simba na Yanga wamewekwa katika Kundi moja pamoja na Dakadaha ya Somalia na Saint George ya Ethiopia.

    Musonye alisema kwamba Kundi A linaundwa na timu za Azam FC, KCCA ya Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator FC ya Sudan Kusini, wakati Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sport ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Djibouti.
    FIFA imeridhia Kagame kufanyika mwezi huu tofauti na agizo lake la kutotaka katika mwezi wa Fainali za Kombe la Dunia yasifanyike mashindano mengine yoyote, kwa sababu washiriki watano wa michuano hiyo wapo kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, ambayo kwa sasa imesimama kupisha Kombe la Dunia itarejea Julai baada ya kumalizika kwa michuano hiyo nchini Urusi.
    Hao ni KCCA ya Uganda iliyopo Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine nne kwenye Kombe la Shirikisho ambazo ni Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda, Yanga ya Tanzania zilizopoi Kundi D zote na Al-Hilal ya Sudan iliyopo Kundi A.
    Na kwa sababu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika itakwenda hadi Agosti, mwezi ambao msimu mpya wa Ligi Kuu nyingi duniani huanza – michuano ya Kagame isipofanyika mwezi huu kuna hatari isifanyike tena na mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo.
    Azam FC ndiyo mabingwa wa mwisho wa michuano hiyo ilipofanyika Tanzania, walipowafunga Gor Mahia 2-0 katika fainali Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya waliokuwa washambuliaji wake hatari, John Raphael Bocco dakika ya 17 na Muivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
    Na hiyo ndiyo ilikuwa michuano iliyomtoa mshambuliaji Mkenya, Michael Olunga ambaye kwa sasa anachezea Girona FC ya Hispania kwa mkopo kutoka Guizhou Zhicheng ya China.
    Baada ya kufunga mabao matano akiwa na Gor Mahia na kuibuka mfungaji bora akiwapiku , Osman Bilal Salaheldin wa Al-Khartoum ya Sudan aliyefunga mabao manne sawa na Tchetche wa Azam FC, Olunga akachukuliwa na Djurgardens IF ya Sweden mwaka 2016 iliyomuuza Guizhou Zhicheng mwaka 2017.
    Siku mbili baadaye, Yanga SC wakasema wameandika barua kujitoa kwenye mashindano hayo, kwa sababu wamebanwa na ratiba ya mashindano mengi kiasi cha kukosa muda wa kupumzika.
    Afisa Habari wa Yanga, Dissmas Ten alisema; “Ni kweli hatutashiriki mashindano ya Kagame Cup kutokana na ratiba kuwa ngumu kwa upande wetu, kumekuwa na msongamano wa mashindano baada ya kumalizika kwa ligi tumeenda Kenya kwenye michuano ya SportSpesa Super Cup, tumerudi majuzi tu hapa,”
    “Pia tuna mechi nyingine ya Kombe la Shirikisho Afrika tutakayocheza nchini Kenya Juni 16 mwaka huu dhidi ya Gor Mahia, hivyo ukiangalia msongamano huo hata wachezaji wetu watakosa muda wa kupumzika, hivyo tumeona ni bora kutoshiriki mashindano hayo ili kuwapa muda wachezaji wetu ili waweze kujiandaa na mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika,”amesema Ten.
    Siku moja baadaye, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akawajibu Yanga akiwapa saa 48 hadi leo kutoa jibu linaloeleweka juu ya kujitoa kwao kwenye michuano hiyo, kwani sababu walizozitoa  hazina mashiko.
    Karia alisema; “Sababu walizozitoa Yanga juu yakutoshiriki michuano ya Kagame hazina mashiko, maana si Yanga peke yao ambao ratiba imewabana na ukiangalia hiyo michuano ya Shirikisho Afrika hata Gor Mahia pia wapo, mashindano ya SportPesa Super Cup ambayo mpaka hivi sasa Gor Mahia wapo na wanacheza fainali Jumapili na Simba,”.
    “Hivyo kabla hata hatujalipeleka suala hili CECAFA, nauomba uongozi wa Yanga hadi kufika jumapili uwe umetoa jibu la kueleweka juu ya mashindano hayo,”amesema Karia.
    Kama Yanga haitashiriki mashindano haya, itaungana na mabingwa wa Sudan, Al-Hilal Omdurman ambayo imejitoa tena bila sababu. Wamesema tu hawashiriki.
    Wakijitoa Yanga hii haitakuwa mara ya kwanza, wamewahi kujitoa ikiwemo mwaka 2000 walipokataa kwenda Kigali nchini Rwanda kutetea taji lao kutokana na kutolipwa fedha zao za zawadi kwa kuwa mabingwa wa mwaka 1999 nchini Uganda.
    Lakini timu nyingi zimekuwa zikijitoa kwenye mashindano hayo kwa taarifa za mapema au tu kutothibitisha, kwa sababu mashindano haya yenyewe yamepoteza hadhi yake ile ya miaka ya kuanzia 1974 inaanzishwa hadi miaka ya 1990.
    Yamekuwa mashindano ambayo kanuni zake hazieleweki kama ilivyo kwa mashindano mengine yote ya CECAFA ikiwemo Kombe la Challenge. Pia hayana tena uhakika wa kufanyika na hayapo katika utaratibu mzuri wa kupokezana uenyeji ni aliye tayari kuwa mwenyeji anaweza kuandaa.
    Yalianzishwa kama mashindano yanayoshirikisha mabingwa wa nchi tu, ikitokea nchi ikawa na timu mbili, basi nyingine ni bingwa mtetezi wa mashindano. Lakini siku hizi mwenyeji anaingiza hadi timu tatu, inakuwa sasa sawa na Kombe la Mapinduzi tu au SportPesa SuperCup na ndiyo maana ninasema mashindano yamepoteza hadhi yake.
    Kinachoonekana mashindano haya hayajapo kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya soka kwa ukanda huu, bali kwa faida ya viongozi wa CECAFA na ndiyo maana katika makundi matatu, timu mbili za Tanzania zimewekwa kundi moja wakati kundi moja halina mwenyeji.
    Kesi za aina hii zikienda hata kwa wenye mpira wao, FIFA watawastaajabu sana hao viongozi wanaofanya madudu ya aina hiyo. Ni aina mpya kabisa duniani ya upangaji wa makundi. Walijifungia watu chumbani wakapanga ratiba yao kwa utashi na maslahi yao, wakagongesha glasi zao, wakaagana kwa furaha na vicheko wakutane tena kwenye mkutano na Waandishi wa Habari.   
    TFF kama wenyeji, ikiwa imepewa fursa ya kuingiza timu tatu, ilipaswa kuwasiliana na klabu zake kujua zipi zipo tayari kwa mashindano haya kwanza – lakini pia katika kutaka kutumia nafasi ya uenyeji kuhakikisha taji linabaki nyumbani, yenyewe ilipaswa kuhakikisha inazitumia vizuri hizo nafasi tatu kwa kuingiza timu bora.
    TFF wanajua matatizo ya Yanga ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na wao wenyewe kuiacha klabu haina Mwenyekiti tangu Mei mwaka jana baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Yussuf Manji kujiuzulu.
    Wachezaji wa Yanga wamegoma kwa sababu wanadai fedha nyingi na wamekwisharejea kwao kupumzika na zikiwa zimebaji wiki mbili michuano kuanza ajabu gani Yanga kutangaza kujitoa?
    Kwa busara, TFF kama baba wa mpira wa miguu nchini inapaswa kukutana na Yanga kwa mazungumzo ya ana kwa ana kujua kwa kuambiwa na muhusika, Waingereza wanasema; “From the horses mouth” juu ya hali halisi ya klabu na kutafuta namna ya kuwasaidia. Kama hawajui, viongozi wa TFF warudi kwenye miongozo yao juu ya majukumu yao watafute nini wajibu wao kama waendeshaji wa mpira wa miguu nchini.
    Na kwa muda uliobaki hakuna sababu ya kuendelea kusumbuana na Yanga – kuna wawakilishi wawili wa michuano ya Afrika mwakani, Simba SC na Mtibwa Sugar wapewe nafasi hizo mbili za ziada iwasaidie kuanza kujenga timu za kushindana kwenye Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa mwakani.   
    Kwa mfano TFF inapolazimisha Yanga ishiriki inajenga picha gani kwa wapenzi wa soka – Karia amewahi kujiuliza? Watu wanajua yeye Karia, Katibu wake, Wilfred Kidau na wajumbe wengi ni wapenzi wa Simba, tuamini haya yanaletwa na unazi wao wa kuichukia Yanga wanataka iende kufedheheka kwa kufungwa mabao mengi?
    Na mashindano haya kwa hali halisi ya Yanga kwa sasa hayana faida kwao kwa sababu mwakani hawaendi popote. Azam aende kama bingwa mtetezi, nafasi nyingine wapewe Simba na Mtibwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA SASA KOMBE LA KAGAME HALINA FAIDA KWA YANGA, ZIFIKIRIWE SIMBA NA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top