• HABARI MPYA

  Sunday, June 03, 2018

  KIPIGO CHAZUA TAFRANI JANGWANI, KIONGOZI AJIUZULU CHUMBANI NA KUWATAKA WENZAKE PIA WANG’OKE WAMETIA AIBU

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga, Salum Mkemi amejizulu leo muda mfupi tu baada ya timu kutolewa katika hatua ya kwanza ya michuano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya. 
  Mkemi ameposti picha akiwa chumbani na kuambatanisha ujumbe usemao; “Kusema kweli viongozi hatukwepi lawama hizi. Kwa hakika tumepata aibu kubwa. Nikiwa kama kiongozi napaswa kuwajibika kwa hili. Ni hatua nzuri ya kupisha mawazo mapya kwa wanachama wengine kuongoza timu na kutupeleka mbele,”.
  Ujumbe huo umeendelea kusema; “Pia ningependa kuwashauri viongozi wenzangu wajitathimini na ikibidi nao waachie ngazi ufanyike uchaguzi mkuu kwa pamoja tupate viongozi wapya kabla msimu mpya haujaanza,”.

  Njooni tulale; Salum Mkemi ameposti picha hii sambamba na waraka wa kujiuzulu Yanga leo

  “Napenda kuomba samahani kwa wote niliowakwaza na nimesamehe wote walio nikikwaza. Naomba kutamka rasmi; ‘Mimi Salum Mkemi Najiuzulu nafasi zangu zote za Uongozi ndani ya klabu yangu pendwa, Young Africans Sports Club "YANGA " kuanzia tarehe ya Leo 03/06/2018,”.  
  “Nawatakia kila la kheri Viongozi wenzangu waliobaki na Kuwataka Radhi tena Wanachama, Wapenzi na Mashabiki wa Yanga kwa Matokeo mabovu tuliyopata naomba tusamehane. Nawashukuru kwa Muda mlionipa kuiongoza Klabu hii kubwa Afrika. Naomba kuwajibika kwa kujiuzulu, wenu mwanachama mwenzenu mtiifu. Salum Mkemi, Nimeng'atuka,”amesema mtangazaji huyo wa zamani w Redio Clouds.
  Hatua ya Mkemi inakuja baada ya Yanga SC kuendelea kuogelea kwenye wimbi la matokeo mabaya, baada ya kutolewa hatua hatua ya kwanza tu ya michuano ya SportPesa Super Cup kufuatia kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Kakamega Homeboyz Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
  Hicho kinakuwa kipigo cha saba katika mechi 14, nyingine saba ikitoa sare sita na kushinda moja tangu kuondokewa na aliyekuwa kocha Mkuu wake, Mzambia George Lwandamina.
  Japokuwa tayari imeleta kocha Mkuu mpya, Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyesaini mkataba wa miaka miwili mwezi uliopita, lakini Yanga imeendelea kuongozwa na waliokuwa makocha Wasaidizi wa Lwandamina, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali.
  Katika mchezo wa leo, mabao ya Kakamega Homeboyz yamwefungwa na mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Allamn Watende Wanga mawili dakika za 26 na 30 na Wycliffe Opondo dakika ya 85, wakati bao pekee la Yanga limefungwa na Matheo Anthony dakika ya 38.
  Na kujiuzulu kwa Mkemi, kunaongeza idadi ya viongozi waliochaguliwa Juni mwaka 2016 kuondoka akiwemo Omary Said Amir wakimfuatia Mwenyekiti, Yussuf Mehboob Manji aliyeondoka Mei mwaka jana.
  Viongozi waliobaki ni Kaimu Mwenyekiti Clement Sanga aliyeshinda Umakamu Juni 2016 na Wajumbe Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Ayoub Nyenzi, Samuel Lukumay, Hashim Abdallah na Hussein Nyika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIPIGO CHAZUA TAFRANI JANGWANI, KIONGOZI AJIUZULU CHUMBANI NA KUWATAKA WENZAKE PIA WANG’OKE WAMETIA AIBU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top