• HABARI MPYA

  Monday, June 11, 2018

  BOCCO AWA MCHEZAJI BORA WA MSIMU SIMBA SC, OKWI MSHAMBULIAJI BORA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Simba SC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa klabu, akiwaangusha wachezaji wenzake, winga Shiza Ramadhani Kichuya na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi.
  Katika hafla iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro, Dar es Salaam, Bocco pia alishinda tuzo ya Bao Bora la Msimu, alilofunga dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.
  Lakini Kichuya na Okwi nao hawakuondoka watupu, kwani mshambuliaji kutoka Uganda alibeba tuzo ya mshambuliaji bora na winga wa kimataifa wa Tanzania akabeba tuzo ya Kiungo Bora. Katika tuzo ya kiungo Bora, Kichuya aliwaangusha Jonas Mkude na Mghana, James Kotei. Okwi naye akawashinda Kichuya na Bocco kuwa mshambuliaji bora.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akimkabidhi John Bocco tuzo ya Mchezaji Bora Msimu
  Gwiji wa klabu, Mtemi Ramadhani (kushoto) baada ya kumkabidhi tuzo ya kiungo Bora, Shiza Kichuya
  Gwiji wa klabu, Abdallah Kibadeni (kushoto) akimkabidhi tuzo ya Mshambuliaji Bora, Emmanuel Okwi 
  Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ally Hassan Mwinyi (kulai) akimkabidhi tuzo ya Mafanikio ya Muda Wote, Suleiman Matola

  Mwanahisa mkuu mtarajiwa wa Simba SC, Mohammed 'Mo' Dewji kulia akiwa na Kaimu Rais wa klabu, Salim Abdallah na Waziri Kigwangala pamoja na Bocco 

  Aishi Manula akawaangusha Said Mohamed 'Nduda' na Emmanuel Elias Mseja kuwa kipa bora, Erasto Nyoni akawashinda Yusuph Mlipili na Shomari Kapombe kuwa beki bora, Zainab Rashid Pazi akawashinda Rukia Salum na Dotto Makunja kuwa Mchezaji Bora wa Kike. 
  Rashid Juma akawashinda Salum Shaaban na Ally Salim kuwa Mchezaji Bora Chipukizi na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi akamkabidhi tuzo ya Heshima kwa Mafanikio ya Muda Wote, kiungo na kocha wa zamani wa klabu, Suleiman Abdallah Matola.
  Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ akatunukiwa tuzo ya Kiongozi Bora wa Msimu, marehemu Fihi Salehe Kambi akatunikiwa tuzo ya Shabiki Bora wa Msimu, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ akawashinda Salama Jabir, Mbunge Zitto Kabwe, mwigizaji Vyonne Cherrie ‘Monalisa’ na mwimbaji mwenzake, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ kushinda tuzo ya Mhamasishaji Bora kwenye Mitandao.
  Msemaji wa timu, Haji Manara akashinda tuzo ya Mhamasishaji Bora wa Jumla akimuangusha Mzee Muchacho, shabiki wa miaka mingi wa Simba SC na Ubungo Terminal likashinda tuzo ya Tawi Bora la Msimu likiyashinda matawi ya Wazo Hill na Vuvuzela.
  Kukatolewa tuzo maalum za benchi la Ufundi zilizokwenda kwa Kocha Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre, Msaidizi wake, Mrundi, Masoud Djuma, Kocha wa Mazoezi ya Viungo Mtunisia Aymen Mohamed Hbibi, kocha wa makipa Muharami Mohamed ‘Shilton’, Meneja Richard Robert, Daktari Yassin Gembe na Mratibu Abbas Selemani.
  Ikatolewa pia tuzo ya Wasimamizi wa mchakato wa mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu kuingia kwenye soko la Hisa, ambayo walikabidhiwa Jaji Mstaafu Thomasi Mihayo, Wakili Damasi Ndumbaro, Abdulrazak Badru, Mussa Hassan Zungu, Yusuph Nassoro, Brenda Mrema na Mzee Hamis Boma.
  Wengine ni Revocatus Cosmas Sangu, Hashim Nyendage, Gervas Alpha Honest, Emmanuel Metusela Urembo, Mulamu Nghambi, Suleiman Omari, Aziz Kifile, Salim Abdallah Muhene, Arnold Kashembe, Omari Bakari Mtika na Evodius Mtawala.
  Tuzo hizo zilizoandaliwa na mwanahisa mkuu mtarajiwa wa klabu, Mohammed 'Mo' Dewji, zilihudhuriwa na Rais Mstaafu Mwinyi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na mwanamuziki nyota, Nassib Abdul ‘Diamond’ aliyemkabidhi tuzo rafiki yake, Hajji Manara.
  Ikumbukwe, Simba imemaliza msimu vizuri kwa mataji mawili, Ngao ya Jamii na ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOCCO AWA MCHEZAJI BORA WA MSIMU SIMBA SC, OKWI MSHAMBULIAJI BORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top