• HABARI MPYA

    Monday, June 11, 2018

    BENKI YA NBC YAMPELEKA MANJI MAHAKAMANI KWA DENI LA SHILINGI BILIONI 26

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imemshitaki mfanyabiashara, Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji na wengine wanne kwa kushindwa kulipa mkopo wa Sh. Bilioni 26.
    Kwa mujibu wa gazeti la Serikali, Daily News la leo NBC imemfungulia mashitaka Manji na wenzake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashra madai ya kwanza ni juu ya Farm Equip (Tanzania) Company Limited, na Manji na watu wengine wanaosimama kama wadhamini.
    Wadaiwa wengine katika mkopo huo ni ni pamoja na Tanperch Limited, Quality Group Limited na Kaniz Manji. Mkopo wa pili ulikwenda kwa Tanperch Limited, ikiripotiwa umedhaminiwa na Manji, Quality Group Limited na Kaniz Manji, ambao pia ni wahusika.

    Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji na wengine wanne kwa wameshitakiwa kwa deni la Sh. Bilioni 26

    Kwa mujibu wa barua ya Mahakama iliyochapishwa kwenye vyombo vya Habari hivi karibuni, watuhumiwa wote katika mikopo hiyo miwili wanatakiwa kufika Mahakamani wao wenyewe au kutuma Mawakili wao Juni 25, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
    Katika kuchukua mikopo hiyo mali zisizohamishika, ikiwemo ardhi na majengo ziliwekwa kama dhamana ikiwa ni pamoja viwanja vitatu vilivyopo eneo la Ilemela mjini Mwanza, ambavyo vimesajiliwa kwa jina la Tanperch Limited.
    Dhamana nyingine ni jengo liliopo eneo la Sea View mjini Dar es Salaam kwa jina la Quality Group Limited ambavyo vyite vitaingizwa mnadani kufidia madeni ya Farm Equip (Tanzania) Company Limited.
    Na haya yanakuja siku moja baada ya wanachama wa klabu ya Yanga kukubaliana kumrejesha madarakani,  Manji katika mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam aliyejiuzulu Mei mwaka jana.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BENKI YA NBC YAMPELEKA MANJI MAHAKAMANI KWA DENI LA SHILINGI BILIONI 26 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top