• HABARI MPYA

  Wednesday, June 06, 2018

  AZAM FC YAITA WACHEZAJI WAKE KAMBINI HARAKA MAANDALIZI YA KOMBE LA KAGAME

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  AZAM FC itaingia kambini Juni 15, mwaka huu kuanza maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame Cup katika michuano inayotarajiwa kuanza Juniu 28 hadi Julai 13, mwaka huu mjini Dar es Salaam.
  Azam FC imelazimika kufupisha muda wa mapumziko ya wachezaji wake baada ya msimu, kufuatoa jana Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kutoa ratiba ya michuano ya Kagame na sasa wachezaji wote wanatakiwa kuripoti Juni 15 kuanza kazi chini ya kocha mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm.
  Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi Maganga amesema kwamba wamefurahia michuano hiyo itafanyika mjini Dares Salaam na watatumia fursa ya kucheza nyumbani kutetea Kombe.

   “Kutokana na ujio wa michuano ya Kombe la Kagame, likizo ya wachezaji wa Azam FC imefupishwa ambapo watarejea kuuanza msimu mpya (pre season) Juni 15 mwaka huu chini ya Kocha Mpya, Hans Van Pluijm,”.
  Jaffar amesema kwamba wanatarajia michuano itakuwa migumu kama ilivyo kawaida, lakini watajipanga vizuri ili wabebea tena Kombe hilo.   
  Azam FC, wanatarajia kuanza kutetea ubingwa huo kwa kuvaana na Kator FC ya Sudani Kusini mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Juni 29 mwaka huu saa 10.00 jioni.
  Azam FC ilitwaa ubingwa huo Agosti 2, 2015 hapa nchini wakati michuano hiyo ilipofanyika kwa mara ya mwisho, ikiifunga Gor Mahia mabao 2-0, yaliyofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco 'Adebayor', aliyehamia Simba msimu huu na Kipre Tchetche, anayecheza soka la kulipwa nchini Malaysia hivi sasa.
  Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kushirikiana na wenyeji Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadhamini Kampuni ya Azam TV jana wametoa ratiba ya michuano hiyo itakayokuwa na timu 12 zilizogawanywa katika makundi matatu.
  Azam FC ipo Kundi A pamoja na Kator FC ya Sudan Kusini, JKU ya visiwani Zanzibar na KCCA ya Uganda, ambayo imeibuka mabingwa wa nchi hiyo msimu huu.
  Mara baada ya Azam FC kufungua dimba na Kator, itashuka tena dimbani Julai Mosi kuvaana KCCA ya Uganda Saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex kabla ya kumalizia hatua ya makundi kwa kukipiga na JKU Julai 4 saa 1.00 usiku.
  Kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo itakayoshirikisha timu 12, Katibu Mkuu wa CECAFA Nicholaus Musonye, ameeleza kuwa timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu kwa hatua ya robo fainali pamoja na timu bora mbili zilizoshika nafasi ya tatu zilizopata matokeo mazuri (best looser).
  Bingwa wa michuano hiyo, anatarajia kuweka kibindoni kitita cha Dola za Marekani 30,000 (sawa na zaidi ya Sh milioni 62 za Tanzania), mshindi wa pili Dola 20,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 42 za Tanzania) na mshindi wa tatu Dola 10,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 22 za Tanzania).
  Musonye amedokeza kuwa huenda kitita hiko kikaongezeka kama wadhamini wakijitokeza kwa wingi kudhamini mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya pili mfululizo jijini Dar es Salaam.
  Wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba na Yanga, wamepangwa Kundi C pamoja na St. George ya Ethiopia na Dakadaha ya Somalia huku Kundi B likiundwa na Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic ya Burundi na Ports  ya Djibout.
  Azam FC ilitwaa Kagame mwaka 2015 kwa rekodi ya aina yake, bila kupoteza mchezo wowote wala kuruhusu bao katika mechi zote sita ilizocheza, ikizifunga KCCA 1-0, Al- Malakia 2-0 na Adama City 5-0 kwenye hatua ya makundi na kufuzu robo fainali.
  Mabingwa hao wakaiongoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia suluhu ndani ya dakika 120, ikaifurusha KCCA kwa bao 1-0 kwenye nusu fainali kabla ya kuikung’uta Gor Mahia (2-0) katika fainali na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAITA WACHEZAJI WAKE KAMBINI HARAKA MAANDALIZI YA KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top