• HABARI MPYA

    Sunday, June 17, 2018

    AZAM FC YAENDELEA KUJIUMBA UPYA, YASAJILI BONGE LA BEKI LA UGANDA

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imezidi kujiimarisha kuelekea msimu ujao, baada ya kumsajili beki hodari wa kimataifa wa Uganda, Nicholas Wadada.  
    Beki huyo wa kulia na Nahodha wa kikosi cha wachezaji wa nyumbani wa The Cranes amesaini miaka miwili kujiunga na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na faimilia yake akitokea Vipers ya kwao.
    Kulikuwa kuna habari kwamba, Wadada aliyeng’ara katika Ligi Kuu ya Uganda alikuwa anatakiwa na klabu kadhaa za Afrika Kusini na kwa kutua wake Azam FC maana yake timu ya Chamazi imelamba dume.
    Meneja wa Azam FC, Philipo Alando (kulia) akimkabidhi jezi ya Nico Wadada baada ya kusaini 


    Wadada mwenye umri wa miaka 23, amekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda tangu mwaka 2012 na hadi sasa amekwishaichezea The Cranes mechi 46 na pamoja na kwamba ni mlinzi, lakini pia amefunga bao moja.
    Wadada anakuwa mchezaji mpya wa tatu wa kigeni kusajiliwa Azam FC kuelekea msimu mpya, baada ya Wazimbabwe, kiungo Tafadzwa Kutinyu kutoka Singida United na mshambuliaji Donald Ngoma kutoka Yanga.
    Lakini kwa ujumla, Wadada anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa Azam FC kuelekea msimu ujao, kwani pamoja na Kutinyu na Ngoma, timu hiyo pia imewasajili wazawa kiungo Mudathir Yahya anayerejea nyumbani baada ya kucheza kwa mkopo Singida United msimu uliopita na Ditram Nchimbi kutoka Njombe Mji FC iliyoshuka Daraja.
    Ikumbukwe Azam FC msimu ujao itakuwa chini ya benchi jipya la Ufundi, Kocha Mkuu, Mholanzi Hans van der Pluijm kutoka Singida United na Msaidizi wake, mzalendo Juma Mwambusi ambao misimu miwili iliyopita walifanya kazi pamoja kwa mafanikio Yanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAENDELEA KUJIUMBA UPYA, YASAJILI BONGE LA BEKI LA UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top