• HABARI MPYA

  Thursday, June 07, 2018

  ADUI NAMBA MOJA WA YANGA NI UONGOZI ULIOPO MADARAKANI, SI WAZIRI DK. MWIGULU NCHEMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  UJUMBE unasambazwa kwenye makundi ya wapenzi na wanachama wa Yanga ukimtuhumu, Rais wa Singida United, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi kwamba anaifanyia ubaya klabu hiyo.   
  Yanga wanadai Waziri Mwigulu amekuwa akifuatilia wachezaji ambao klabu hiyo inataka kuwasili na kuwashawishi wahamie Singida United.
  Wanadai amekwishafanya hivyo kwa Tibar John ambaye amesajiliwa Singida United wiki iliyopita kutoka Ndanda FC ya Mtwara na sasa anataka kufanya tena hivyo kwa mshambuliaji kutoka Benin, Marcellin Koukpo.
  Ujumbe huo unamchonganisha Mwigulu na wana Yanga ukitaka kuwaaminisha wapenzi na wanachama wa klabu hiyo eti Waziri huyo ni adui yao.

  Rais wa Singida United, Dk Mwigulu Nchemba (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa timu, Sanga Festo

  Ikumbukwe umaarufu wa Mwigulu katika michezo ulianzia Yanga baada ya kujipambanua kama mpenzi na mwanachama wa klabu hiyo.
  Baadaye katika kuchangia maendeleo ya soka mkoani mwake na kujiweka karibu na wapiga kura wake, Mwigulu akawa sehemu ya urejeo wa timu ya Singida United ambayo ndiyo hii sasa inayosumbuana na Yanga.
  Akiwa Rais wa klabu, Mwigulu ni mtu wa juu sana ambaye kutokana pia na majukumu yake ya Kiserikali hajihuhusishi na shughuli za kila siku za uendeshwaji wa Singida United, bali anauachia uongozi chini ya Mwenyekiti, Yussuf Mwandami na Watendaji kama Mkurugenzi, Sanga Festo.
  Na Mwigulu hajawahi kuruhusu Singida United isajili mchezaji wa Yanga, labda wale ambao waliachwa akina Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deus Kaseke pamoja na kocha Hans van der Pluijm.
  Pamoja na kuwa Rais wa Singida United, Mwiguku amebaki kuwa mwanachama na mpenzi wa Yanga, ambaye bado yupo kwenye makundi ya klabu na anatoa michango yake. Kana kwamba hiyo haitoshi, anaumia vile vile na matokeo mabaya ya timu.
  Lawama ambazo anatengenezewa sasa hivi ni kujaribu kutaka kuuficha udhaifu wa klabu unaotokana na viongozi wake wasiofaa iliyonao nao sasa.
  Yanga imeshindwa kufanya lolote kwa sasa na ni kwa sababu ya aina ya viongozi iliyonao sasa ambao wanatakiwa kuondoka haraka, ikibidi hata sasa ili ufanyike uchaguzi wa kupata viongozi wapya.
  Yanga wanaposema Mwigulu kamuiba Tibar John wanakuwa wanasema uongo, kwa sababu klabu haikuwahi kuingia mkataba na mchezaji huyo.
  Singida United walikuwa wanamtaka Adam Salamba na waliposikia Yanga wanamtaka pia wakaachana naye, lakini leo mchezaji huyo ni mali ya Simba. Kabla ya kufikiria kuwahadaa wana Yanga eti Mwigulu anataka kumuiba Benin, Marcellin Koukpo – kwanza viongozi waseme ukweli juu ya usajili wa beki Mkongo, Fiston 'Festo' Kayembe Kanku. Naye kaibiwa na Singida?  
  Yanga wameshindwa kumsajili ‘Yanga damu’ Mrisho Ngassa japo akawaongezee nguvu kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup wanataka kuficha udhaifu wao kwa kumpaka matope Nchemba.
  Yanga SC wameshindwa kukaa na wachezaji waliopo klabuni tu kwa sasa kiasi cha kusababisha migomo ya mara kwa mara kwa sababu za kimaslahi. Viongozi wa Yanga wanaweza nini? Labda kumsafirisha Omar Kaaya kwenye mechi za nje ya nchi wakimuacha Ofisa Habari wa klabu, Dissmas Ten.  
  Zaidi ya hapo wanaweza nini? Waseme. Ukweli ni kwamba adui namba moja wa Yanga kwa sasa ni uongozi uliokosa mipango, fikra, mawazo hata ujanja wa kimjini tu kuipeleka klabu katika wakati huu mgumu.
  Yanga ni timu kubwa ina wapenzi kwenye timu nyingine zote zinazoshiriki Ligi Kuu ikiwemo Simba, ina wapenzi hadi pale TFF ambako panaonekana pametawaliwa na watu wa Msimbazi. Wapo Yanga pale akina Athumani Nyamlani, Jemadari Said, Danny Msangi, Baraka Kizuguto na wengine ambao wanaweza kuisaidia timu yao kwa namna moja au nyingine kadiri ya uwezo wao, bila kuvunja sheria au kukiuka miiko ya kazi.
  Inahitajika mipango na ujanja wa kuweza kufika kwa watu kuomba misaada katika kipindi hiki kigumu, kitu ambacho viongozi wa sasa wa Yanga bahati mbaya hawana. 
  Umefika wakati watu wa Yanga waache kuoneana haya, waambiane ukweli kwa manufaa ya klabu, vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya.

  Beki Mkongo, Fiston 'Festo' Kayembe Kanku alisaini Yanga dirisha dogo Januari lakini hajaonekana tena. Yupo Singida?  

  Yanga inaweza kwenda kuchukua wachezaji wa mkopo timu yoyote nchini na ikapewa kama suala ni kuwatumia katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho tu, ligi ikianza warejee timu zao, lakini hadi leo wameshindwa kwa sababu viongozi hawaelewi, hawajielewi na hawaeleweki.
  Viongozi wajanja waliingia Simba SC mwaka 1998 na wakapewa Alphonce Modest, Shaaban Ramadhani na Monja Liseki wacheze hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika – hawa wa sasa wanaweza nini.
  Jumapili Yanga imefungwa kwa mara ya saba katika mechi 14, nyingine saba ikitoa sare sita na kushinda moja tangu kuondokewa na aliyekuwa kocha Mkuu wake, Mzambia George Lwandamina. Hizo ndizo rekodi zinazowekwa chini ya uongozi huu.
  Japokuwa tayari imeleta kocha Mkuu mpya, Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyesaini mkataba wa miaka miwili mwezi uliopita, lakini Yanga imeendelea kuongozwa na waliokuwa makocha Wasaidizi wa Lwandamina, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali. Sababu ni Mwigulu?
  Wanachama na wapenzi wa Yanga wapuuze propaganda za kuwachonganisha na Mwigulu, tena huyo ni mtu muhimu kwa ustawi wa klabu. Kitu ambacho wana Yanga wanapaswa kuimba sasa ni uchaguzi. Unahitajika uchaguzi haraka mno klabu ipate viongozi wapya walete matumaini mapya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ADUI NAMBA MOJA WA YANGA NI UONGOZI ULIOPO MADARAKANI, SI WAZIRI DK. MWIGULU NCHEMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top