• HABARI MPYA

    Thursday, May 03, 2018

    YONDAN ASIMAMISHWA KWA KUMTEMEA ‘MIKOHOZI’ ASANTE KWASI...MANARA AONYWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI tegemeo wa Yanga SC, Kelvin Patrick Yondani, maarufu kwa jina la utani ‘Cotton Juice’ amesimamishwa kwa muda usiojulikana kucheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kosa kumtemea mate beki Mghana wa Simba SC, Asante Kwasi katika mechi ya mahasimu jadi Aprili 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Clement Sanga ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Yanga kupitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu, na malalamiko ya klabu za Yanga na Arusha FC na kuyafanyia uamuzi.
    Katika mchezo ambao bao pekee la beki Erasto Edward Nyoni liliipa Simba SC ushindi wa 1-0, Yondan anadaiwa kumtemea mate Kwasi kwa na kusimamishwa kumezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
    Kelvin Yondan (kulia) amesimamishwa kwa muda usiojulikana kwa kosa kumtemea mate Asante Kwasi  

    Aidha, Kamati hiyo imempa onyo kali Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara  kwa kuingia uwanjani kushangilia ushindi wa timu yake baada ya mchezo kumalizika. 
    “Kitendo chake ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo,”imesema Taarifa ya Bodi ya Ligi.
    Katika hatua nyingine, Mbeya City imepigwa faini ya Sh. 500,000 kutokana na vurugu za mashabiki wake ikiwemo kurusha mawe na chupa uwanjani katika mechi dhidi ya Yanga SC Aprili 22, mwaka huu Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya timu hizo zikitoka sare ya 1-1. 
    Taarifa ta Kamati imesema kwamba adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Kamati pia imeiandikia barua klabu ya Yanga ikiiagiza kumuonya mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa kwa kurudia matukio ya utovu wa nidhamu kwenye mechi za timu hiyo.
    “Kwa vile mchezaji Obrey Chirwa wa Yanga alionywa kwa kadi ya njano kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Mbeya City ingawa kwenye picha za televisheni inaonekana kama alipiga kiwiko, Kamati haikutoa adhabu nyingine kwa vile tayari ameadhibiwa,”.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YONDAN ASIMAMISHWA KWA KUMTEMEA ‘MIKOHOZI’ ASANTE KWASI...MANARA AONYWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top