• HABARI MPYA

  Thursday, May 03, 2018

  YANGA WANYIMWA, LAKINI ARUSHA FC WAPEWA POINTI ZA MEZANI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imeipa Arusha FC ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya African Sports kuchezesha wachezaji wawili waliotumia leseni za kughushi (non qualified) katika mechi ya Kundi B Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL) baina ya timu hizo Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga hivi karibuni.
  Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Clement Sanga.
  Na Uamuzi huo dhidi ya African Sports umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(17) na 42(23) za Ligi Daraja la Pili. Nayo Arusha FC imepewa ushindi kwa kuzingatia Kanuni ya 14(36) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo. 
  Vilevile viongozi wa African Sports waliohusika kughushi leseni zilizotumiwa na wachezaji hao ambao hawakusajiliwa watafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.
  Aidha, Kamati imekataa malalamiko ya Yanga kutaka ipatiwe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu dhidi ya Mbeya City kwa timu hiyo kuwa na mchezaji zaidi kwenye mechi, kwa vile hakuna Kanuni yoyote ya Ligi Kuu inayoweza kubadili matokeo ya uwanjani kwa mazingira hayo.
  Hakuna namna yoyote ile mchezaji anayezidi (extra player) kubadili matokeo ya mchezo. Katika mazingira ya extra player likifungwa bao, Mwamuzi atalikataa bao hilo. Kutokana na kanuni za Ligi kutojitosheleza katika suala hilo la extra player, Kamati iliangalia Kanuni za FIFA na kufikia uamuzi huo.
  Mchezaji Ramadhan Malima wa Mbeya City ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini akatoka kwenye chumba cha kuvalia (dressing room) kwenda kushangilia bao la kusawazisha la timu yake amesimamishwa hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu TFF. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
  Kwa upande wa waamuzi, kulikuwa na upungufu katika suala la kusimamia ubadilishaji wa wachezaji (substitution), hivyo Kamati ya Waamuzi ya TFF imeandikiwa barua ili ichukua hatua dhidi ya wahusika. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WANYIMWA, LAKINI ARUSHA FC WAPEWA POINTI ZA MEZANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top