• HABARI MPYA

    Wednesday, May 02, 2018

    YANGA SC YAFUTA MKUTANO MKUU WA MWAKA ULIOPANGWA KUFANYIKA JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MKUTANO Mkuu wa mwaka wa klabu ya Yanga SC uliopangwa kufanyika Jumamosi wiki hii mjini Dar es Salaam umeahirishwa kutokana na sababu ambazo haziwezi kuzuilika.
    Habari kutokana ndani ya Yanga zimesema kwamba viongozi wengi wa klabu wanasafiri na timu nchini Algeria, ambako Jumapili timu itakuwa na mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.   
    Yanga Sc inatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Algiers kwa ndege ya Emirates Air ikipitia Dubai tayari kwa mchezo huo wa kwanza wa Kundi D Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya U.S.M. Alger Jumapili.
    Pamoja na Yanga na USM Alger, timu nyingine katika Kundi D ni Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya ambazo zitamenyana zenyewe katika ufunguzi wa hatua ya 16 Bora ya Kombe Shirikisho Afrika.
    Clement Sanga amekuwa akikaimu Uenyekiti wa Yanga SC tangu Yussuf Manji aondoke Mei mwaka jana

    Baada ya mechi ya kwanza ugenini Jumapili, Yanga itamenyana na Rayon Sport mjini Dar es Salaam Mei 16 na itakamilisha mechi za mzunguko wa kwanza kwa kuwafuata Gor Mahia mjini Nairobi Julai 18.
    Mzunguko wa pili Yanga itaanzia nyumbani Julai 29 na Gor Mahia, kabla ya kuwakaribisha na USMA Alger Agosti 19 na kwenda kumalizia ugenini Agosti 29 na Rayon.
    Ikumbukwe Yanga imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji Mei mwaka jana.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Hali hiyo ilisababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufadhili Yanga na kufanya wachezaji wakose mishahara kwa kipindi chote hicho kabla ya viongozi wenzake kuanza kufanya jitihada za kulipa taratibu.
    Pamoja na kuwepo kwa wadhamini, kampuni za SportPesa, Macron, Azam TV na maji ya Afya, lakini bado imeendelea kuripotiwa hali ya kifedha si nzuri ndani ya klabu na hayo ndiyo yalitarajiwa kujadiliwa kwa mapana marefu Mei 5.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAFUTA MKUTANO MKUU WA MWAKA ULIOPANGWA KUFANYIKA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top