• HABARI MPYA

  Wednesday, May 02, 2018

  SUNDAY SHOMARI: TULIPATA TABU KUITAMBULISHA BONGO FLEVA MIAKA YA 90

  Na Mwandishi Wetu, WASHINGTON DC
  SIKU chache baada ya Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ kufungua kituo chake cha televisheni cha Wasafi TV – Ali Kiba alifunga ndoa ya kifahari iliyoambatana na sherehe kubwa iliyorushwa 'live' na Azam TV kuanzia Mombasa, nyumbani kwa wakwe na baadaye Dar es Salaam ambako pia alizindua kinywaji chake (energy drink) cha MoFaya.
  Hawa ni wasanii wa muziki wa Bongo Fleva wenye mafanikio walioanza kutikisa kwenye medani ya muziki huo mwanzoni mwa muongo huu nchini.
  Na ndiyo wanamuziki wawili wakubwa zaidi wa muziki huu wa vijana, wakiwagawa mashabiki wa Bongo Fleva katika makundi mawili -- Team Kiba na Team Diamond.
  Ni muziki ambao sasa unawakilishwa hadi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako taifa linawashuhudia magwiji wawili wa Bongo Fleva, Joseph Osmund Mbilinyi na Joseph Haule wakiwa na madaraka makubwa ya kisiasa.
  Sunday Simba Patrick Shomari akiwa kazini VOA 
  Sunday Shomari (kulia) akiwa na Mary Mgawe ambaye wanafanya naye kazi VOA katika kipindi cha Duniani Leo 'DL' kwa sasa baada ya awali kufanya kazi pamoja ITV 
  Sunday Shomari (kushoto) akiwa na mkewe,  Elinita (kulia) na watoto wao, Rose na Ernest.
  Sunday Shomari akiwa kazini VOA hivi karibuni nchini Marekani

  Mbilinyi enzi zake akijulikana kwa majina kama 2 Proud, Mr. II, Sugu na sasa Jongwe ni Mbunge wa Mbeya Mjini, wakati Haule enzi zake alijulikana kama Nigger Jay kabla ya sasa kwenda kwa jina la kisanii la Profesa Jay, yeye ni Mbunge wa jimbo la Mikumi, wote kupitia tiketi ya chama kikuu cha upinzani, Chadema.
  Siyo siasa tu, Bongo Fleva sasa ina wasomi na wajasiriamali wakubwa. Ambwene Yessayah ‘AY’, mkongwe mwingine wa Bongo Fleva, ni mjasiriamali maarufu wakati Hamisi Mwinjuma 'MwanaFA' ni ofisa wa zamani wa benki. Muziki huo una heshima kubwa kabisa hivi sasa.
  Lakini miaka 20 na ushei iliyopita, wakati Bongo Fleva inaanza kutambulishwa kama muziki rasmi, hali ilikuwaje?
  Sunday Simba Patrick Shomari ni miongoni mwa watangazaji wa mwanzoni wa Redio na Televisheni walioupigania muziki huo kusimama kwanza kama muziki kamili, wakifuata nyayo za Taji Liundi ‘Master T’, ambaye inaaminika ndiye ‘Baba wa Bongo Fleva’. 
  Na katika mahojiano na Bin Zubeiry Sports – Online wiki hii nchini Marekani, Sunday Shomari ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Sauti la Amerika (VOA) anasema; “Tulipata wakati mgumu sana kuutambulisha huu muziki kwenye vyombo vya Habari, ulichukuliwa kama wa kihuni na wanaoimba ni wahuni, ila tulisimama kidete kuhakikisha muziki huu unasimama,”.
  “Na sasa Bongo Fleva ni kitu kikubwa sana. Ni fahari ya kipekee kabisa!! Ni kama ndoto vile,” anaongeza Sunday Shomari ambaye kwa mwaka wa 10 sasa ni mtangazaji wa VOA tangu aondoke Redio One na ITV ambako ndiko aliupigania muziki wa Bongo Fleva.
  Ingawa Radio One & ITV Sunday Shomary alipoingia mwaka 1995 alikuwa maarufu kwa vipindi vya sanaa na burudani, lakini VOA anafanya vipindi mbalimbali vya habari na uchunguzi.
  Sunday Shomary bado ni raia wa Tanzania, ambaye kuhusu kufanya kazi Marekani akiwa mgeni anasema; “Hainigharimu kufanya kazi Marekani, nikiwa raia wa kigeni kwa sababu kuna wanaofanya kwa visa na wanaofanya kazi na green card, ambao ni wakazi, hivyo mimi ni mkazi ninayemiliki Green Card”.
  Sunday ni mume wa Elinita waliyebahatika kupata naye watoto wawili, Rose mwenye umri wa miaka sita na Ernest mwenye miaka minne ambao watakapofikisha umri wa miaka 18 watachagua kuwa raia wa Tanzania au Marekani walipozaliwa kwa mujibu wa sheria.
  Mara baada ya kujiunga na Redio One mwaka 1995 alianza kutangaza kipindi cha Salamu, baadaye Reggae Time kabla ya kuingia kwenye kipindi kilichompa umaarufu zaidi cha Chombeza cha usiku.
  “Mimi niliingia Redio One na kuanza kutangaza moja kwa moja baada ya wiki chache tu, nakumbuka niliingia pamoja na Mike Mhagama na Peace Kwiyamba. Nilianza na kipindi cha Salamu, baadaye Reggae Time na Chombeza,” anasema Sunday.
  Baadaye Sunday akawa anatangaza na kwenye Televisheni pia, vipindi vya muziki kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.
  Japokuwa yupo Marekani kwa mwaka wa 10 sasa, lakini Sunday Shomari bado anafuatilia muziki wa Tanzania na anasema anavutiwa na wasanii wengi wakiwamo Kiba, Diamond, Profesa Jay, Mwana FA, AY pamoja na wanaoinukia kama Mary Angel.
  Sunday Shomary mzaliwa wa Upanga, Dar es Salaam, aliyepata elimu zake za Msingi katika shule za Arusha na Muhimbili kabla ya kujiunga na sekondari za Forodhani baadaye na Almuntazir, mwaka 1996 alikwenda Marekani kwa masomo ya Uandishi wa Habari ambako alitunukiwa Cheti katika Utangazaji wa TV mjini Washington DC.
  Na akiwa ITV alisomea Uandishi wa Habari chuo cha TSJ mwaka 1998, wakati mwaka 2005 alisomea Teknolojia ya Mawasiliano (IT) nchini Marekani na kutunukiwa Cheti na kwa sasa anaendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Maryland anakochukua Shahada ya Mawasiliano.
  Miongoni mwa vipindi anavyofanya VOA ni pamoja na Duniani Leo ‘DL’, Let’s Talk cha Kiingereza katika Redio na Washington Bureau ‘WB’ kinachorushwa kwenye Televisheni ambacho pia hurushwa na Televisheni ya Star TV ya nyumbani.
  Pamoja na kufanya kazi VOA, Sunday Shomary amekuwa akifanya kazi za uongozaji wa shughuli, maarufu kama MC na anasema amesafiri majimbo mengi Marekani kwa ajili ya harusi za Watanzania na raia wengine wakiwamo Wamarekani pia.
  “Na moja ya shughuli za kukumbukwa katika kumbukumbu zangu ni kuwa MC mbele ya mabalozi wa Afrika kwenye siku ya kimataifa ya Umoja wa Afrika (AU) hapa Washington Juni 12, mwaka jana wakisherehekea miaka 54 ya kuzaliwa kwa umoja huo”.
  Lakini pia, Sunday anasema kwamba katika shughuli za VOA, moja ya kazi anazozikumbuka alizowahi kupangiwa ni kuripoti uchaguzi wa kihistoria wa Marekani uliomuweka madarakani Barack Obama 2008 na pia uchaguzi uliomuweka madarakani Donald Trump.
  Baada ya kuwa mtangazaji mkubwa ni ipi ndoto nyingine Sunday Shomary bado hajatimiza katika maisha yake?
  “Ni kusaidia watu wa kijijini kwetu Bonde, Tanga wapeleke maisha yao katika ngazi nyingine, tuwe na shule nzuri, hospitali na huduma muhimu kama hizo. Kwa nchi zetu ukifanya hivyo wengi wanafikiria siasa, ila mimi nimejifunza haya Marekani, kila mtu anayefanikiwa maishani au Mungu akimjaalia kidogo apatacho anawasaidia na kule alikoanzia,” anasema.
  Sunday Shomari anamtaja bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa uzito wa juu duniani, Muhamad Ali, sasa marehemu kama shujaa wake. “Ali pamoja na ukubwa wake wote, lakini alisema maisha ya hapa duniani ni mafupi mno, yanapita tu bora kuangalia yaliyo muhimu na hakuwa na majivuno na alisimamia haki,” anasema Sunday.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SUNDAY SHOMARI: TULIPATA TABU KUITAMBULISHA BONGO FLEVA MIAKA YA 90 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top