• HABARI MPYA

  Sunday, May 06, 2018

  SIMBA SC KUENDELEZA SHANGWE ZA UBINGWA TAIFA LEO…INAKIPIGA NA NDANDA FC ILIYOJICHOKEA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC leo wanatarajiwa kuendeleza shangwe zao katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salam.
  Simba SC imebakiza pointi sita kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu ambazo inahitaji kuzipata kwenye mechi zake za leo na Aprili 13 dhidi ya wenyeji, Singida United Uwanja wa Namfua.
  Ili mipango yake iende sawa, timu hiyo iliyo chini ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia Mohamed Aymen Hbibi, Mrundi Masoud Juma na mzawa Muharami Mohammed kocha wa makipa inahitaji kushinda.
  Pamoja na kwamba Ndanda FC ipo kwenye hatari ya kushuka haitarajiwi kwa namna yoyote kuizuia Simba SC kuendeleza na shangwe zake za kuelekea kukabidhiwa taji lao la kwanza la ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2012.
  Wakati Simba SC ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 62 baada ya mechi 26, ikifuatiwa kwa mbali na Azam FC yenye pointi 49 za mechi 26 pia, mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 48 za mechi 24, Ndanda FC wanashika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu ya timu 16 wakiwa na pointi 23 za mechi 26, mbele ya Njombe Mji FC yenye pointi 22 za mechi 27.    
  Ikumbukwe timu mbili zitateremka mwishoni mwa msimu na tayari timu sita zimekwishapanda ambazo ni African Lyon, KMC, JKT Tanzaniaza Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara ili kupata timu 20 msimu ujao.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Maji Maji FC wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Kagera Sugar FC wataikaribisha Mbeya City FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Stand United FC wataikaribisha Azam FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Ikumbukwe mechi mbili zimechezwa jana, Singida United ikishinda 4-0 dhidi ya Njombe Mji FC, mabao ya Kambale Salita dakika ya 42, Miraj Juma dakika ya 60 kwa penalti, Lubinda Mundia dakika ya 62 na Nizar Khalfan dakika ya 90 na Tanzania Prisons ikishinda 1-0 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa  Sokoine mjini Mbeya bao pekee la Laurian Mpalile dakika ya tisa limeipa ushindi wa 1-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUENDELEZA SHANGWE ZA UBINGWA TAIFA LEO…INAKIPIGA NA NDANDA FC ILIYOJICHOKEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top