• HABARI MPYA

  Friday, May 04, 2018

  RUVU SHOOTING NA MWADUI FC MECHI YA AINA YAKE YA LIGI KUU MABATINI LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja tu, Ruvu Shooting FC wakiikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
  Ruvu wataingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 3-1 na Maji Maji mjini Songea Aprili 28 katika mchezo wao uliopita, wakati Mwadui walishinda 1-0 nyumbani dhidi ya Mbao FC Aprili 29.
  Wakiwa nyumbani leo, Ruvu timu iliyotemwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na sasa inamilikiwa na watu binafsi, watahitaji ushindi ili kutafuta kumaliza kwenye nafasi za juu katika msimamo wa Ligi Kuu.  
  Kwa upande wao, Mwadui FC nao watahitaji ushindi wa ugenini ili pia kutafuta kumaliza kwenye nafasi ya juu zaidi katika msimamo wa Ligi Kuu inayoelekea ukingoni.  
  Ikumbukwe Ruvu Shooting inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya timu 16, ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Mwadui FC katika nafasi ya tisa, ambayo ina pointi 29 za mechi 26 pia. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa michezo miwili, Singida United FC wakiikaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Namfua na Tanzania Prisons FC wakiwa wenyeji wa Lipuli FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Na Jumapili Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, wenyeji Maji Maji wataikaribisha Mtibwa Sugar, Kagera Sugar FC wataikaribisha Mbeya City FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Stand United FC wataikaribisha Azam FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Simba SC watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RUVU SHOOTING NA MWADUI FC MECHI YA AINA YAKE YA LIGI KUU MABATINI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top