• HABARI MPYA

  Sunday, May 06, 2018

  OKWIIII……NDANDA WAFA 1-0 TAIFA, SIMBA SC YABAKIZA POINTI TATU KUTANGAZA UBINGWA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  BAO pekee la mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya 43 limetosha kuipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Okwi alifunga bao lake la 20 la msimu katika Ligi Kuu baada ya kutanguliwa pasi ndefu na kiungo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia, Shomari Kapombe na kumhadaa beki wa Ndanda FC, Hemed Khoja kabla ya kumtungua kwa shuti la mbali kipa Diel Makonga.
  Simba SC inafikisha pointi 65 baada ya ushindi huo katika mechi yake ya 27 na itahitaji kushinda mchezo wake ujao dhidi ya Singida United Uwanja wa Namfua Mei 13 ili kutawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu. 
  Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kuifungia Simba bao pekee leo


  Emmanuel Okwi akimtoka beki wa Ndanda FC, Ayoub Masoud 
  Nahodha wa Simba SC, John Bocco akimuacha chini beki wa Ndanda FC, Ayoub Masoud  
  Kiungo wa Simba, Shomari Kapombe akimtoka kiungo wa Ndanda FC, Majid Bakari
  Kiungo mshambuliaji wa Ndanda FC, Mrisho Ngassa akiwatoka wachezaji wa Simba SC

  Ndanda FC wanazidi kukaribia kurudi Ligi Daraja la Kwanza baada ya kipigo hicho, wakibaki na pointi zao 23 baada ya mechi 27 wakiwa katika nafasi ya 15 kwenye Ligi ya 16, itakayoteremsha timu mbili mwishoni mwa msimu.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka wa Arusha, aliyesaidiwa na Makame Mdogo wa Shinyanga na Sylvestre Mwanga wa Kilimanjaro pamoja na kufungwa, Ndanda FC walioongozwa na kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa walicheza vizuri.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Nicholas Gyan/Rashid Juma dk62, Asante Kwasi/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk72, James Kotei, Yusufu Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi/Laudit Mavugo dk90, John Bocco na Shiza Kichuya.
  Ndanda: Daniel Makonga, William Lucian, Ayoub Masoud, Ibrahim Job, Hemed Khoja/Baraka Majogoro dk80, Jacob Masawe, Salum Minely, Majid Bakari, Omar Mponda/Nassor Kapama dk74, Mrisho Ngassa na Tiba John/Ahmed Msumi dk84.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Maji Maji FC imelazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, sawa na Kagera Sugar FC waliotoka pia 0-0 na Mbeya City FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati Stand United FC wameshinda 2-1 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Mabao ya Stand United yamefungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 75 na Ali Ali dakika ya 90 wakati la Azam FC limefungwa na Shaaban Iddi Chilunda dakika ya 76.
  Maji Maji inajiongezea pointi moja na kufikisha 24 baada ya mechi 27, ingawa inabaki nafasi ya 14, wakati Kagera Sugar inafikisha pointi 28 za mechi 27 na inabaki nafasi ya 12, Mbeya City inafikisha pointi 29 za mechi 27 inabaki nafasi ya 11 wakati Stand United inapanda hadi nafasi ya tisa kutoka ya 10 ikifikisha pointi 32 katika mechi ya 27.
  Mtibwa Sugar inabaki nafasi ya sita baada ya kufikisha pointi 34 na Azam FC inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake 49 za mechi 27, nyuma ya mabingwa watarajiwa, Simba SC na mbele ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 48 za mechi 24.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWIIII……NDANDA WAFA 1-0 TAIFA, SIMBA SC YABAKIZA POINTI TATU KUTANGAZA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top