• HABARI MPYA

    Thursday, May 03, 2018

    MTIBWA SUGAR YATAKA KUENDELEZA REKODI YA KUITESA MAJI MAJI POPOTE

    Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
    TIMU ya Mtibwa Sugar SC inaondoka leo kwa basi lake kwenda Songea mkoani Ruvuma tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Maji Maji FC JUmapili Uwanja wa Maji Maji mjini humo.
    Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila ambaye ni mchezaji wa zamani wa klabu hiyo amesema kwamba wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu wanakwenda kucheza ugenini, lakini watapambana wapate ushindi.
    “Ukiachilia mbali hiyo ya kucheza ugenini, lakini wapinzani wetu (Maji Maji) wanapigana vita ya kuepuka kushuka Daraja, kwa hiyo watacheza kwa nguvu sana leo. Mchezo utakuwa mgumu,”amesema Katwila. 
    Mtibwa Sugar inashika nafasi ya sita kwa sasa katika Ligi Kuu ya timu 16 kutokana na pointi zake 33 za mechi 25, wakati Maji Maji ni ya 14 kutokana na poniti zake 23 za mechi 26 na inatakiwa kujiondoa kwenye eneo hilo la hatari.
    Lakini kitakwimu Mtibwa Sugar wamekuwa wababe wa Maji Maji katika Ligi Kuu, kwani katika mechi saba zilizopita ambazo timu hizo zimekutana Wakata Miwa hao wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro wameshinda tano, kufungwa moja na sare moja.
    Na katika michezo hiyo saba, Mtibwa Sugar wamefanikiwa kufunga jumla ya mabao tisa, huku Maji Maji wao wakizitikisa nyavu za wapinzani wao hao mara tano.
    Katika michezo hiyo saba, waliyokutana katika Ligi Kuu hadi sasa, mitatu ilichezwa kwenye Uwanja wa Maji Maji na Mtibwa Sugar imeshinda michezo miwili na kupoteza mmoja.
    Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho, Ruvu Shooting FC wakiikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, wakati Jumamosi kutakuwa na michezo miwili, Singida United FC wakiikaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Namfua na Tanzania Prisons FC wakiwa wenyeji wa Lipuli FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mbali na Maji Maji na Mtibwa Sugar, mechi nyingine za Jumapili Kagera Sugar FC wataikaribisha Mbeya City FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Stand United FC wataikaribisha Azam FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Simba SC watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YATAKA KUENDELEZA REKODI YA KUITESA MAJI MAJI POPOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top