• HABARI MPYA

    Friday, May 04, 2018

    KARIA ATIA UBANI MICHUANO YA LIGI YA MABINGWA WA MIKOA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Wallace Karia amezitakia kila la heri timu zote 28 zinazoanza kibarua cha kutafuta nafasi ya kupanda daraja kutoka katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa(RCL) inayotarajia kuanza Mei 6 na kumalizika Mei 22,2018 kwenye vituo vinne.
    Karia amezitaka timu zote kupambana uwanjani na wachezaji kuzingatia nidhamu ili kuongeza ushindani wa mashindano hayo na kupata matokeo mazuri yatakayoziwezesha kufikia lengo la kupanda daraja,huku akisisitiza timu zote kufuata sheria na kanuni za mashindano.
    Karia amewataka waamuzi watakaochezesha mashindano hayo katika vituo vyote vinne kuzingatia haki na sheria za Mpira wa miguu bila hiyari ili kuwapata washindi sahihi wanaostahili na pia Waamuzi wenyewe kujiweka katika nafasi ya kuangaliwa maendeleo yao na uwezekano wa kupandishwa katika madaraja ya juu.
    Rais wa TFF, Wallace Karia amezitakia kila la heri timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa 

    Aidha, Rais huyo amewataka viongozi wote wanaohusika na wasimamizi kusimamia haki na kuhakikisha sheria na kanuni zinafuatwa pasipo upendeleo na dhuluma kwa yeyote.
     “Nasisitiza kwa timu zote,viongozi,wasimamizi na waamuzi kufuata sheria, kanuni na taratibu za mashindano tunahitaji kuona ushindani kutoka kwao ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni na taratibu za mashindano lakini waamuzi nao wachezeshe kwa haki kwa kufuata sheria za mpira wa miguu,TFF tutakuwa wakali kwa yeyote atakayekwenda kinyume na sheria,kanuni na taratibu za mashindano”.amesema Rais wa TFF Ndugu Karia.
    Ligi ya RCL itakayoshirikisha timu 28 itachezwa katika vituo vinne vya Geita,Rukwa,Singida na Kilimanjaro kila kituo kikiwa na kundi moja lenye timu 7.
    Timu 2 za juu kutoka kila kundi zitapanda daraja kwenda kucheza Ligi Daraja la Pili msimu unaofuata wakati timu zitakazosalia katika kila kundi zitarejea kucheza Ligi katika mikoa yao.
    Wakati huo huo: Rais wa TFF, Wallace Karia amepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa viongozi wawili wa timu ya Mwena FC ya Mtwara Mjumbe wa kamati ya Utendaji Steven Abdallah na daktari Hashim Sued kilichotokea Mei 1,2018 kwa ajali ya gari.
    Karia amesema ni mshtuko mkubwa kupokea taarifa za msiba huo wa kupoteza viongozi hao wawili kwa wakati mmoja.
    “Nimeshtushwa sana na taarifa hizi na kwa niaba ya TFF natoa pole kwa familia zao,Ndugu,Mwenyekiti wa Mwena FC Benedict Macheso,familia ya mpira wa miguu,Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mtwara na marafiki kwa msiba huo mzito wa kupoteza viongozi wawili kwa wakati mmoja hakika ni masikitiko makubwa kwetu na wana familia kiujumla”.Amesema Karia.
    Amewataka wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na TFF inaungana nao katika kuomboleza msiba huo.
    Ajali iliyosababisha vifo vya viongozi hao wa Mwena FC ilitokea eneo Chikukwe wakati timu hiyo ikitokea kucheza mchezo wa kirafiki Newala kujiandaa na Ligi ya Mabingwa wa Mikoa inayoanza Mei 6,2018 timu hiyo ikiwa kituo cha Kilimanjaro.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA ATIA UBANI MICHUANO YA LIGI YA MABINGWA WA MIKOA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top