• HABARI MPYA

    Sunday, April 15, 2018

    YANGA YAONDOKA BILA AJIB KWENDA ETHIOPIA MECHI YA MARUDIANO NA WOLAITA DICHA JUMATANO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Ibrahim Ajib hayumo kwenye kikosi cha mabingwa wa Tanzania, Yanga SC kilichoondoka Alfajiri ya leo kwenda Hawassa, Ethiopia tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumatano dhidi ya wenyeji, Wolaita Dicha.
    Kikosi cha wachezaji 20 na viongozi 13 kimepanda ndege ya shirika la Ethiopia kwena Addis Ababa baadaye kuunganisha usafiri wa barabara kwenda Hawassa kufuata tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Wachezaji waliosafiri Alfajiri ya leo ni makipa; Youthe Rostand, Beno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Haji Mngwali, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’,  Kelvin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavario, viungo; Papy Tshishimbi, Yussuf Mhilu, Raphael Daudi, Pius Buswita, Geoffrey Mwashiuya, Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi na Emmanuel Martin wakati washambuliaji ni Obrey Chirwa, Yohana Mkomola na Thabani Kamusoko, wakati Ajib ameachwa kwa sababu anaumwa Malaria.
    Ibrahim Ajib hayumo kwenye kikosi cha Yanga SC kilichoondoka Alfajiri ya leo kwenda Ethiopia 

    Yanga watakuwa wageni wa Wolaita Dicha Jumatano jioni Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa wakitoka kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
    Lakini katika mchezo huo wa marudiano ambao Yanga wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi wao kwenye mchezo wa kwanza, hawatakuwa na kocha wao Mkuu, Mzambia, George Lwandamina aliyeondoka mapema Jumanne kwenda kukamilisha mipango ya kurejea Zesco United ya kwao.
    Zesco United imeamua kumrejesha kocha wake huyo baada ya mafanikio yake Tanzania ndani ya miaka miwili, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita na sasa inakaeribia kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.
    Kwa sasa benchi la Ufundi la Yanga lipo chini ya walimu watatu waliokuwa Wasaidizi wa Lwandamila, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAONDOKA BILA AJIB KWENDA ETHIOPIA MECHI YA MARUDIANO NA WOLAITA DICHA JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top