• HABARI MPYA

  Wednesday, April 18, 2018

  YANGA WAFUZU HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA NA KUJINYAKULIA MAMILIONI YA CAF

  Na Mwandishi Wetu, HAWASSA
  YANGA SC imefanikiwa kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na kufungwa 1-0 na wenyeji, Wolaita Dicha katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika jioni ya leo Uwanja wa Kimataifa wa Hawassa mjini Hawassa nchini Ethiopia.
  Yanga SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Aprili 7 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC imejihakikishia dola za Kimarekani 150,000, zaidi ya Sh. Milioni 300 kwa kuingia tu hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambazo zinaweza kuongezeka hadi dola 239 000, karibu Sh. Milioni 500 ikimaliza nafasi ya tatu au ya pili kwenye kundi lake.
  Ikitwaa Kombe itapata dola 625,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.2 na ikimaliza nafasi ya pili itapata dola 432,000 karibu Sh. Bilioni 1.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa Ali Sabila, Mark Ssonko na Balikoowa Musa Ngobi wote wa Uganda, hadi mapumziko Wolaita Dicha walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wake kutoka Togo, Arafat Djako dakika ya pili tu akimalizia kona ya chini chini iliyowapita mabeki wa Yanga na kumkuta upande wa nguzo ya mwisho ya goli na kufunga kwa guu la kulia.
  Baada ya bao hilo, Wolaita waliongeza kasi ya mashambulizi na kuutawala kwa mchezo kwa pasi zao za haraka haraka za hapa na pale, lakini Yanga ilisimama imara kuokoa hatari zote.
  Sifa zimuendee kipa Mcameroon, Youthe Rostand aliyeokoa michomo miwili ya hatari kipindi cha kwanza baada ya makosa ya mabeki wake.
  Beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alikaribia kuifungia Yanga dakika ya 44 kwa kichwa baada ya kona ya beki Hassan Ramadhani  Kessy kutoka upande wa kulia.
  Kipindi cha pili, Dicha waliendelea kushambulia zaidi langoni mwa Yanga, ambao waliendelea kucheza kwa tahadhari.
  Kwa ujumla zifa zimuendee Rostand aliyeendelea kuokoa vizuri na kuisaidia timu hiyo kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu. 
  Yanga SC ilianzia kwenye Ligi ya Mabingwa ambako ilotolewa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1 iliyofungiwa nyumbani, Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam Machi 6 kabla ya kwenda kutoa sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
  Katika Raundi ya Awali, Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe.
  Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
  Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
  Mara ya kwanza Yanga kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
  Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
  Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
  Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
  Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers. 
  Kikosi cha Wolaita Dicha kilikuwa; Wondwosen Babsa, Teklu Kumma, Zelelem Wolebo, Yared Yarfo, Arafat Djako, Tesfu Eyamo, Amrala Arsicha, Bezabih Mekengo, Eyob Alanbo, Eshetu Mena Medelecho na Haymanot Tesfaye.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Abdallah Shaibu Ninja, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi/Emmanuel Martin dk68, Obrey Chirwa, Thabani Kamusoko/Said Juma ‘Makapu’ dk51, Raphael Daudi, Pius Buswita na Yussuf Mhilu.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAFUZU HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA NA KUJINYAKULIA MAMILIONI YA CAF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top