• HABARI MPYA

  Tuesday, April 17, 2018

  YANGA SC IPO KAMILI HAWASSA TAYARI KUWAANGAMIZA WOLAITA DICHA JUMATANO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA imejipanga kufanya vizuri katika mchezo wa wa marudiano dhidi ya Dicha ya Ethiopia utakaopigwa Jumatano mjini Hawassa, nchini humo.
  Kikosi cha mabingwa hao wa Tanzania kiliwasili salama Jumatatu na kufikia katika hoteli nzuri ya Rori Holiday ambayo mazingira yake ni rafiki kukaa wachezaji.
  Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa siku kutoka Hawassa leo kwamba kikosi cha timu hiyo kipo vizuri na jana asubuhi walitumia muda wa saa moja kufanya mazoezi ya kutembea katika mitaa mbalimbali ya mji huo kwa ajili ya kuweka miili yao sawa kabla ya jioni kufanya mazoezi ya uwanjani.
  “Tupo vizuri hakuna shaka lolote tumepokewa vizuri hakuna figisu figisu zozote zlitokea kwa kweli tumepata faraja kubwa sana kuona kuna Watanzania wenzetu huku wanatupa sapoti imebaki kazi moja tu ya uwanjani kupata matokeo,” alisema Hafidh.
  Alisema katika kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wa timu hiyo, Kocha Noel Mwandila ambaye amekabidhiwa mikoba ya George Lwandamina tangu wamefika nchini humo amekuwa akitumia muda mwingi kuongea na wachezaji wake kuhusiana na mchezo huo wa kesho na kuwandaa kisaikolojia.
  “Kimsingi wachezaji wamekuwa wakiandaliwa zaidi kisaikolojia,” aliongeza Hafidh.
  Kikosi cha wachezaji 20 na viongozi 13 kipo mjini Hawassa kufuata tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Wachezaji waliopo huko ni makipa; Youthe Rostand, Beno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Haji Mngwali, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’,  Kelvin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavario, viungo; Papy Tshishimbi, Yussuf Mhilu, Raphael Daudi, Pius Buswita, Geoffrey Mwashiuya, Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi na Emmanuel Martin wakati washambuliaji ni Obrey Chirwa, Yohana Mkomola na Thabani Kamusoko.
  Yanga watakuwa wageni wa Wolaita Dicha Jumatano jioni Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa wakitoka kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
  Lakini katika mchezo huo wa marudiano ambao Yanga wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi wao kwenye mchezo wa kwanza, hawatakuwa na kocha wao Mkuu, Mzambia, George Lwandamina aliyeondoka mapema Jumanne ya wiki iliyopita kwenda kukamilisha mipango ya kurejea Zesco United ya kwao.
  Zesco United imeamua kumrejesha kocha wake huyo baada ya mafanikio yake Tanzania ndani ya miaka miwili, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita na sasa inakaeribia kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.
  Kwa sasa benchi la Ufundi la Yanga lipo chini ya walimu watatu waliokuwa Wasaidizi wa Lwandamila, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC IPO KAMILI HAWASSA TAYARI KUWAANGAMIZA WOLAITA DICHA JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top