• HABARI MPYA

  Sunday, April 15, 2018

  MAZURI MILIONI 100 YA LWANDAMINA YANGA YANAVYOFUTWA NA HILI MOJA TU!

  JUMANNE wiki hii kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina aliondoka kurejea kwao kujiunga tena na klabu yake ya zamani, Zesco United.
  Lwandamina ambaye mkataba wake unamalizika Juni mwaka huu, aliondoka Yanga siku moja kabla ya kuteremka uwanjani kumenyana na Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao timu hiyo ilitoa sare ya 1-1.  
  Lwandamina alijiunga na Yanga Novemba mwaka 2016 akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na katika kipindi hicho ameiongoza timu katika michezo 77 ya mashindano yote akitoa sare 18, kushinda 45 kati ya hizo mbili kwa penalti baada ya sare ndani ya muda wa kawaida na kufungwa 14, tano kwa penalti baada ya sare katika muda wa kawaida.
  Bahati mbaya sana, Lwandamina aliingia Yanga wakati wa neema ya ufadhili wa Yussuf Manji, ambaye alijiuzulu Uenyekiti Mei mwaka jana na tangu hapo klabu imekuwa katika hali ngumu kiuchumi, wachezaji na makocha wakikaa muda mrefu bila kulipwa mishahara.
  Wakati wote, Lwandamina ndiye aliyekuwa akiwasihi wachezaji kutofanya migomo na kuingia kucheza pamoja na hali ngumu. Wakati fulani ikaripotiwa Lwandamina amemuondoa kundini kipa, Benno Kakolanya kwa sababu aligoma kushinikiza apewe mkataba mpya badala ya kuendelea kucheza huku akisubiri suala la mkataba wake linafanyiwa kazi.   
  Nilimuona Lwandamina ni kocha wa kipekee sana. Kuna wakati iliripotiwa Lwandamina alikataa kupokea malipo ili wapewe wachezaji. Nilimuona mtu mwema sana. Na kweli, pamoja na hali ngumu ya kiuchumi inayoripotiwa, Yanga inafanya vizuri kuliko watani wao, Simba SC ambao wanaripotiwa wanaogelea kwenye bahari ya neema.
  Yanga bado ipo kwenye michuano ya Afrika, Simba imekwishatolewa. Yanga SC ilifika Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), Simba SC ilitolewa hatua ya 64 Bora. Yanga bado ipo kwenye mbio za ubingwa nyuma ya Simba SC na mechi chache zilizosalia zitaamua.
  Taswira ya Lwandamina wakati wote imekuwa ni kocha mvumilivu, muungwana na aliyejua kuishi na wachezaji wake.  Wakati fulani, Lwandamina alipata misiba mfululizo, kwanza akifiwa na baba yake mzazi, baadaye mwanawe na wachezaji wa Yanga walihuzunika sana.
  Lwandamina alichukuliwa ni zaidi ya kocha mbele ya wachezaji wa Yanga, walimuona kama baba. Lakini ajabu, Jumatatu alikuwa nao mazoezini na akaagana nao kana kwamba wangekutana Jumanne na kumbe ndiyo siku ambayo alipakia mizigo yake yote kwenye ndege kurejea kwao.
  Hakuwaaga wachezaji wake. Walizisikia habari za kuondoka kwake kwenye vyombo vya Habari. Wazi iliwaumiza sana kwa sababu hakuna walichomkosea kocha wao huyo hadi kuwafanyia alivyowafanyia. Wamepigana msimu mzima katika mazingira magumu kulinda heshima ya mwalimu wao huyo. 
  Walisimama kimya kwa dakika moja mbele ya umati wa mashabiki uwanjani kabla ya mechi kuomboleza msiba wa kocha wao mara mbili huku wamejifunga vitambaa vyeusi mikononi. Waliuona ukamilifu wao pale tu walipokuwa na Lwandamina.
  Yote hayo Lwandamina hakuyazingatia na sikushangaa hata Yanga ilipotoa sare katika mchezo ambao wangeweza kushinda, bila shaka tu kwa msongo wa mawazo baada ya mtu waliyemuona kama baba yao kuondoka bila kuwaaga. 
  Lwandamina alishindwa kusubiri japo baada ya mechi na Singida United ndiyo aage na kuondoka? Leo Lwandamina anaweza kukubali hakumtendea haki Kakolanya? 
  Mbele ya mashabiki wa Yanga, Lwandamina alikuwa na thamani kubwa saba, lakini sishangai mazuri yake yote Milioni 100 yakazimwa na kosa moja la namna alivyoondoka Yanga. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAZURI MILIONI 100 YA LWANDAMINA YANGA YANAVYOFUTWA NA HILI MOJA TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top