• HABARI MPYA

    Wednesday, April 18, 2018

    KILA LA HERI YANGA SC; MUNGU IBARIKI TIMU YETU IFUZU HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO

    Na Mwandishi Wetu, HAWASSA
    YANGA SC inateremka Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa, Ethiopia kuanzia Saa 10:00 jioni ya leo kwa saa za Tanzania kumenyana na Welaita Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa marudiano wa mchujo kuwania tiketi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Yanga inaingia kwenye mchezo wa leo, ikiwa na mtaji wa ushindi wa mabao 2-0 iliyooupata kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Aprili 7, mwaka huu.
    Lakini tu, kocha aliyeiongoza Yanga kupata ushindi huo, George Lwandamina amekwishaondoka amerejea klabu yake ya zamani, Zesco United na sasa timu ipo chini ya waliokuw wasaidizi wak Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazawa Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali, kocha wa makipa.
    Katika mchezo wa leo, Yanga itaongezewa na nguvu na wachezaji wake wanne waliokosekana kwenye mechi ya kwanza sababu ya adhabu za kadi za njano, mabeki Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Obrey Chirwa.
    Wolaita Dicha nayo itaongezewa nguvu na wachezaji wao wawili, Teklu Tefesse Kumma na Eshetu Mena Medelecho baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kila mmoja katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Zamalek ya Misri.
    Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake, wakati Yanga SC imetolewa Ligi ya Mabingwa baada ya kufungwa 2-1 na Township Rollers ya Botswana Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam Machi 6 katika mchezo wa kwanza wa 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kwenda kupata sare ya 0-0 kwenye mechi ya marudiano mjini Gaborone nchini Botswana.
    Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
    Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
    Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
    Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
    Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
    Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
    Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
    Mshindi wa jumla atajihakikishia kitita cha dola za Kimarekani, 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1 za Tanzania ambazo zinaweza kuongezeka kama timu ikiingua Nusu Fainali na kuwa dola 800,000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.6), Dola Milioni 1.2 (zaidi ya Sh. Bilioni 2.5) kwa nafasi ya pili na Dola Milioni 2.5 (zaidi ya Sh. Bilioni 5) kwa kuchukua Kombe.
    Matokeo mazuri zaidi kwa timu za Tanzania katika michuano hii ni mwaka 1993, Simba SC ilipofika fainali katika mfumo wa zamani wa mtoano mwanzo hadi mwisho na kufungwa na Stella Abidjan kwa mabao 2-0 Dar es Salaam baada ya sare ya 0-0 nchini Ivory Coast.
    Kila la heri Yanga SC. Mungu ijaalie Yanga SC ishinde mechi ya leo na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI YANGA SC; MUNGU IBARIKI TIMU YETU IFUZU HATUA YA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top