• HABARI MPYA

  Saturday, March 17, 2018

  YANGA YAKOMAA NAO GABORONE, SARE 0-0 WAHAMIA KOMBE LA SHIRIKISHO

  Na Mwandishi Wetu, GABORONE
  YANGA SC imeondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Township Rollers jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Gaborone nchini Botswana.
  Matokeo hayo yanamaanisha Rollers inakwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza historia hiyo kwa ushindi wa jumla wa 2-1 uliotokana na matokeo ya mchezo wa kwanza Dar es Salaam Machi 6.
  Yanga SC sasa wanaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako watamenyana na moja ya timu zilizofuzu hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo.
  Sifa zimuendee kipa Mcameroon, Youthe Rostand wa Yanga aliyeokoa michomo kadhaa ya hatari na kuwanyima mabao wenyeji.
  Rostand aliyekuwa benchi kwenye mchezo wa kwanza Yanga ikichapwa 2-1, leo alianzishwa badala ya kipa aliyedaka Dar es Salaam, Ramadhan Kabwili na kuonyesha uwezo mkubwa.
  Leo Kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina alimuanzishia benchi kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib, huku akiwaanzisha marasta, viungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
  Tatizo kubwa la Yanga leo limeendelea kuwa safu ya ushambuliaji hususan katika kipindi hiki ambacho inawakosa Mzimbabwe, Donald Ngoma na Mrundi Amissi tambwe huku, Mzambia Obrey Chirwa akicheza chini ya kiwango chake kwa sasa.   
  Kocha Msaidizi wa Yanga, Nsajigwa Shadrack alipandishwa jukwaani dakika ya 85 baada ya kujibizana na refa Redouane Jiyed wa Morocco.
  Kikosi cha Township Rollers FC kilikuwa; Keeagile Kgosipula, Tshepo Motlhabankwe, Simisani Mathumo, Mosha Gaolaolwe, Edwin Olerile, Motsholetsi Sikele, Maano Ditshupo, Lemponye Tshireletso/Ntesanya Simanyan dk90, Segolame Boy, Edwin Moalosi na Joel Mogorosi/Ivan Ntege dk84.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Pius Buswita/Juma Mahadhi dk90, Thabani Kamusoko/Ibrahim Ajib dk62 na Yussuf Mhilu/Geoffrey Mwashiuya dk69.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAKOMAA NAO GABORONE, SARE 0-0 WAHAMIA KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top