• HABARI MPYA

  Tuesday, March 06, 2018

  YANGA WEPEESIII, WAGONGWA 2-1 NA TOWNSHIP ROLLERS KAMA WAMESIMAMA TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Township Rollers ya Botswana imetanguliza mguu mmoja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji, Yanga SC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Rollers watakuwa na kazi nyepesi tu wiki ijayo watakaporudiana na Yanga mjini Gaborone ili kujihakikishia tiketi ya kwenda hatua ya 16 Bora ya mashindano, ambayo huchezwa kwa makundi, kila kundi likiundwa na timu nne.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Pacifique Ndabihawenimana aliyesaidiwa na Willy Habimana na Pascal Ndimunzigo wote wa Burundi, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
  Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Juma Mahadhi aijaribu kupiga mpira mbele ya wachezaji wa Township Rollers 
  Wachezaji wa Township Rollers wakishangilia bao lao la pili
  Ivan Ntege wa Township Rollees akikimbilia mpira dhidi ya Emmanuel Martin wa Yanga
  Tshepo Motlhabankwe wa Rollers akijaribu kuuwahi mpira dhidi ya Ibrahim Ajib wa Yanga (kulia)
  Mfungaji wa bao la Yanga, Obrey Chirwa akimuacha chini mchezaji wa Rollers

  Na ni wageni ndio waliotangulia kupata bao dakika ya 10 tu kupitia kwa Lemponye Tshireletso kwa shuti la umbali wa mita 20 baada ya kumchungulia kipa kijana mdogo wa miaka 18, Ramadhani Kabwili na kuukwamisha mpira nyavuni kiulaini.
  Yanga wakasawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliji wake Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 30 akimalizia pasi nzuri ya kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi.
  Kipindi cha pili Yanga inayofundishwa na kocha Mzambia, George Lwandamina ilikianza vizuri na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Rollers, lakini bahati ya kufunga bao tu ndiyo walikosa.
  Pamoja na kupoteza nafasi mbili nzuri, mshika kibendera namba moja, Willy Habimana alikataa bao lililofungwa na kiungo Pius Charles Buswita akimalizia krosi ya Mwashiuya akidai alikuwa ameotea.
  Yanga waliongeza juhudi ya kushambulia langoni mwa Rollers jambo ambalo liliwagharimu kufungwa bao la pili kwa shambulizi la kujibiwa dakika ya 83 kupitia kwa Motsholetsi Sikele.
  Yanga walipoteza mwelekeo baada ya bao hilo na kama Rollers wangekuwa makini wangenenepesha ushindi wao.
  Sasa Yanga inatakiwa kwenda kushinda 2-0 ugenini siku 10 zijazo ili kuingia hatua ya makundi, vinginevyo itaangukia kwenye kapu la kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.  
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondani, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Pato Ngonyani, Ibrahim Ajib/Juma Mahadhi dk68, Obrey Chirwa na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk64.
  Township Rollers; Keeagile Kgosipula, Maano Ditshupo, Mosha Gaolaolwe, Simisani Mathumo, Tshepo Motlhabankwe, Kaone Vanderwesthuisen, Motsholetsi Sikele, Lemponye Tshireletso, Segolame Boy, Mthokozisi Msomi/Ivan Ntege dk44 na Joel Mogorosi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WEPEESIII, WAGONGWA 2-1 NA TOWNSHIP ROLLERS KAMA WAMESIMAMA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top