• HABARI MPYA

  Tuesday, March 06, 2018

  YANGA WAWANIA BILIONI 1.1 ZA CAF LEO…NI MZIGO WATAPATA WAKIITOA TU TOWNSHIP ROLLERS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC leo inaingia kwenye mtihani wa kwanza wa kuwania Dola za Kimarekani 550,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.1 iwapo wataingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Wana Dar es Salaam hao leo wanawakaribisha Township Rollers ya Botswana katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Jijini kuanzia Saa 10:00 jioni. 
  Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kutokana na ukweli kwamba, Yanga watakutana na timu nzuri, Rollers iliyoiondoa mashindano El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda 3-0 Gaborone na kwenda kufungwa 2-1 Khartoum.
  Yanga SC yenyewe ilipita kwa mbinde hatua hii, ikishinda 1-0 Dar es Salaam na kwenda kupata sare ya 1-1 Mahe, Shelisheli mbele ya Saint Louis Suns United. 
  Habari njema kwa Yanga leo tu ni kwamba, kiungo mtaalamu, Mzimbabwe Thabani Scara Kamusoko aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu sasa yuko fiti na baada ya kufanya mazoezi na wenzake kwa juma zima, anaweza kuwa sehemu ya mchezo wa leo.
  Pamoja naye, viungo wengine, mzawa Juma Mahadhi na Mzambia, Obrey Chirwa ambao wote wamekuwa wakitumika kama washambuliaji kwa sasa kutokana mapungufu ya wachezaji katika idara hiyo nao wote wako fiti baada ya kukosekana kwenye mechi tatu zilizopita.
  Mahadhi alifunga bao pekee la ushindi dhidi ya St Louis kwenye mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Februari 10 baada ya hapo akakosekana katika mchezo wa marudiano siku 10 baadaye kutokana na homa.
  Mahadhi aliye katika msimu wake wa pili Yanga SC tangu asajiliwe kutoka Coastal Union ya Tanga, alifunga bao hilo dakika ya 66 kwa shuti akimalizia kona iliyopigwa na winga Geoffrey Mwashiuya iliyozua kizazaa langoni mwa Saint Louis.
  Mahadhi alifunga bao hilo dakika moja baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib Migomba kama ilivyokuwa kwa mpishi wa bao lake, Mwashiuya ambaye naye alimbadili Emmanuel Martin.
  Chirwa naye baada ya kupiga nje mkwaju wa penalti dakika ya 25 katika mechi ya kwanza dhidi ya Saint Louis kufuatia beki wa Yanga, Hassan Ramadhani Kessy kuangushwa kwenye boksi na Herve Raktoarison akakosekana kwenye mechi ya marudiano pia kutokana na maumivu ya misuli aliyopapata siku hiyo.
  Wawili hao, wote wakakosekana kwenye mechi mbili za ushindi wa 2-1 mfululizo zilizofuata ugenini za mashindano ya nyumbani, dhidi ya Maji Maji katika Azam Sports Federation Cup (ASFC) mjini Songea mkoani Ruvuma na dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.
  Kamusoko yeye kwa mara ya mwisho aliichezea Yanga dhidi ya Maji Maji Septemba 16, mwaka jana mechi ya Ligi Kuu iliyomalizika kwa sare ya 1-1 na tangu hapo amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya mguu.
  Kocha Mzambia George Lwandamina anafahamu umuhimu wa kuvuka hatua hii kwenda hatua ya makundi, kwani huko wachezaji wake wanaweza kupata fedha za kuwafuta jasho baada ya kupitia kipindi kigumu kutokana na hali mbaya ya kifedha inayoikabili klabu kwa sasa. 
  Yanga wakiitoa Township watakwenda hatua ya makundi moja kwa moja ambako kwa mfumo wa sasa ni makundi manne, baadaye Robo Fainali, Nusu Fainali na Fainali. 
  Kwa mujibu wa utaratibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), timu zinazofuzu hatua ya makundi zinajihakikishia kupata Bilioni 1.1 na zinakwenda kuwania fedha zaidi kulingana na matokeo yake kuanzia hatua hiyo.
  Zinazofanikiwa kwenda Robo Fainali zinapata dola 650,000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.3 wakati kwa Nusu Fainali dau linaongezeka hadi dola 800,000, zaidi ya Sh. Bilioni 1.7 na mshindi wa pili wa mashindano hupata Dola Milioni 1.25 zaidi ya Sh. Bilioni 2.5 na bingwa ni dola Milioni 2.5 zaidi ya Sh. Bilioni 3.
  Yanga imewahi kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara moja tu, mwaka 1998 katika mfumo wa zamani wa kuanzia hatua ya Robo Fainali, wakati kwenye Kombe la Shirikisho pia ilifika hatua ya makundi mwaka 2016. 
  Kila la heri Yanga SC. Mungu ibariki Yanga, Mungu ibariki Tanzania. Amin.
  Yanga iliitoa Saint Louis Suns United katika Raundi ya Awali kwa jumla ya mabao 2-1

  ANGA ZA YANGA MAMBO YAKO HIVI
  Leo Jumanne Machi 6, 2018
  Al Ahly (Misri) vs Mounana (Gabon)
  Horoya (Guinea) vs Generation Foot (Senegal)
  Yanga SC (Tanzania) vs Township Rollers (Botswana)
  Etoile du Sahel (Tunisia) vs Plateau United (Nigeria)
  Kesho Jumatano Machi 7, 2018
  Saint George (Ethiopia) vs KCCA (Uganda)
  Zanaco (Zambia) vs Mbabane Swallows (Swaziland)
  Wydad Athletic Club (Morocco) vs Williamsville AC (Ivory Coast)
  Aduana (Ghana) vs ES Setif (Algeria)
  MFM (Nigeria) vs MC Alger (Algeria)
  Gor Mahia (Kenya) vs Esperance (Tunisia)
  AS Togo (Togo) vs El Hilal (Sudan)
  Zesco (Zambia) vs ASEC Mimosas (Cote d’Ivoire)
  TP Mazembe (DRC) vs UD Songo (Msumbiji)
  Difaa Hassan (Morocco) vs AS Vita (DRC)
  Primeiro de Agosto (Angola) vs Bidvest (Afrika Kusini)
  Rayon Sports (Rwanda) vs Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAWANIA BILIONI 1.1 ZA CAF LEO…NI MZIGO WATAPATA WAKIITOA TU TOWNSHIP ROLLERS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top