• HABARI MPYA

  Monday, March 12, 2018

  YANGA WAIKAMATA SIMBA SC LIGI KUU, WAPAA USIKU HUU KUWAFUATA ROLLERS BOTSWANA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuibamiza Stand United mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya ya kocha George Lwandamina anayesaidiwa na Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali kufikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 21.
  Yanga sasa wanalingana kwa pointi na vinara wa muda mrefu msimu huu, Simba SC ingawa mabingwa hao watetezi wamecheza mechi moja zaidi. 
  Katika mchezo wa leo, mabao ya Yanga SC yamefungwa na beki wa Stand United, Ally Ally aliyejifunga, kiungo Ibrahim Ajib na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa.
  Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Yanag bao la tatu leo
  Ibrahim Ajib akifumua shuti leo licha ya juhudi za Vitalis Mayanga wa Stand United kuzuia
  Obrey Chirwa akijaribu kumpita Ally Ally wa Stand United, kulia 
  Juma Mahadhi wa Yanga, (kulia) akimuacha chini Ally Ally wa Stand United
  Beki wa Stand United, Ally Ally akiokoa mpira miguuni mwa Pius Buswita

   Alianza beki Mzanzibari, Ally Ally kujifunga dakika ya saba katika harakati za kuokoa mpira wa kiungo aliyepandishwa kutoka timu ya vijana, Yussuf Mhilu.
  Akafuatia kiungo mshambuliaji mwenye mambo mengi uwanjani, Ibrahim Ajib Migomba kufunga bao la pili dakika ya 12 akimalizia pasi ya Maka Edward na hadi mapumziko, Yanga walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0.
  Kipindi cha pili, Stand United ya kocha Mrundi, Almasi Niyongabo anayesaidiwa na wazalendo Athumani Bilal na Augustino Malindi kocha wa makipa, ilibadilika na kuanza kuichezea Yanga.
  Haikuwa ajabu Stand United, maarufu kama ‘Chama la Wana’ mjini Shinyanga walipofanikiwa bao dakika ya 84 lililofungwa na mshambuliaji wake, Tariq Seif akiunganisha krosi ya Vitalis Mayanga.
  Obrey Chirwa akarejesha ushindi wa tofauti ya mabao mawili Yanga, kwa kufunga bao la tatu dakika ya 85 akimlamba chenga kipa, Mohammed Makaka na kufumua shuti nyavuni kufuatia pasi ya beki Said Juma ‘Makapu’ aliyepanda kusaidia mashambulizi. 
  Baada ya ushindi huo, Yanga SC inatarajiwa kuondoka Saa 10:00 Alfajiri kwenda Botswana kwa ajili ya mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers Jumamosi mjini Gaborone.
  Yanga inahitaji ushindi wa ugenini wa 2-0 baada ya kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyiopita mjini Dar es Salaam ili kwenda hatua ya makundi.      
  Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Said Juma, Kelvin Yondani, Maka Edward, Yussuf Mhilu, Pius Buswita, Obrey Chirwa, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk76 na Ibrahim Ajib/Emmanuel Martin dk76.
  Stand United; Mohamed Makaka, Aron Lulambo, Miraji Maka/Makenzi Kapinga dk79, Ally Ally, Erick Mulilo, Jisend Mathias/Ismail Gambo dk66, Bigirimana Blaise, Abdul Swamad/Sixtus Sabilo dk79, Tariq Seifu, Ndikumana Seleman na Vitalis Mayanga.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAIKAMATA SIMBA SC LIGI KUU, WAPAA USIKU HUU KUWAFUATA ROLLERS BOTSWANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top