• HABARI MPYA

  Thursday, March 15, 2018

  UONGOZI MBAO FC WAKIRI KUTOWALIPA MISHAHARA WACHEZAJI, MAKOCHA MIEZI MIWILI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Mbao FC ya Mwanza umekiri kutolipa mishahara ya wachezaji na benchi la Ufundi kwa miezi miwili, lakini umesema unahangaikia fedha uweze kulipa haraka iwezekanavyo.
  Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa klabu, Solly Zephania Njashi katika mazungumzo na Bin Zubeiry Sports – Online leo asubuhi.
  Njashi amesema kwamba tatizo la mishahara si la Mbao FC pekee kwa sasa, kwani hata klabu kubwa nchini nazo zinapitia kwenye kipindi kama hicho.
  Hata hivyo, Njashi amesema kwamba wapo kwenye jitihada za kutafuta fedha kuhakikisha wanalipa malimbikizo hayo ya mishahara haraka iwezekanavyo.
  “Na tumezungumza na wachezaji wetu vizuri tu, tunaelewana, tumewapa mapumziko, watarudi kambini Ijumaa na nafikiri watakuta mambo safi,”amesema Njashi.
  Lakini Mwenyekiti huyo amesema kwamba kutolipa mishahara kwa miezi miwili kusihusishwe na matokeo mabaya ya timu siku za karibuni. “Mechi nyingi tunazopoteza siku za karibuni ni za ugenini, ambako timu nyingine pia huwa hazipati matokeo mazuri,”amesema.
  Njashi ameviomba vyombo vya Habari kutochochea mgogoro ndani ya timu, kwani Mbao FC wapo shwari na wanajipanga kwa mechi zao zijazo.
  Mbao FC haijashinda mechi hata moja kati ya sita zilizopita tangu mwezi Februari, wakifungwa tano na kutoa sare moja ya 0-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro tena nyumbani Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.   
  Mechi walizofungwa ni dhidi ya Singida United mjini Mwanza 2-1 Februari 7, Simba 5-0 Februari 26 mjini Dar es Salaam, Tanzania Prisons 1-0 Machi 3, Mbeya City 2-1 Machi 7, zote Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Azam FC 2-1 Machi 11 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
  Mara ya mwisho Mbao FC kushinda mechi ilikuwa Februari 4, walipoichapa Kagera Sugar 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.          
  Na kwa sasa Mbao FC inayocheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu wa pili tangu ipande, inashika nafasi ya 13 katika ligi ya timu 16 kwa pointi 19 za mechi 22.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UONGOZI MBAO FC WAKIRI KUTOWALIPA MISHAHARA WACHEZAJI, MAKOCHA MIEZI MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top