• HABARI MPYA

  Wednesday, March 07, 2018

  SIMBA SC YAKATAA UTEJA NYUMBANI, YALAZIMISHA SARE SARE 2-2 NA AL MASRY

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Simba SC na Al Masry ya Misri umemalizika kwa sare ya 2-2 usiku huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Matokeo hayo yanamaanisha Simba SC wanahitaji kwenda kupigania ushindi wa ugenini siku 10 zijazo mjini Cairo, Misri ili kusonga mbele. 
  Mchezo huo ulisimama kwa takriban nusu saa kuanzia dakika ya 83 kufuatia umeme kukatika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam timu hizo zikiwa zimefungana mabao 2-2.
  Emmanuel Okwi wa Simba akimtoka beki wa Al Masry, Mohamed Koffi aliyeanguka chini 

  Nyota wa Al Masry, Mohamed Ahmed ‘Girindo’ akiwa ameruka juu kuuwahi mpira dhidi ya Jonas Mkude wa Simba
  Mshambuliaji Mghana wa Simba, Nicholaus Gyan akimtoka Ahmed Abdalraof 'Shokry' wa Al Masry 
  Shiza Kichuya wa Simba akimtoka beki wa Al Masry, Islam Salem 
  Islam Atta wa Al Masry akimfunga tela beki Mghana wa Simba, Asante Kwasi  

  Refa Hando Helpus aliyesaidiwa na Zakjele Thusi na Athenkosi Ndongeni wote kutoka Afrika Kusini alilazimika kusimamisha mchezo huo baada ya umeme kukatika ghafla dakika ya 83, dakika 10 tu baada ya Simba kusawazisha bao la pili.
  Wakati huo, tayari mvua kubwa ilikwishaanza kunyesha Uwanja wa Taifa na kusababisha baadhi ya mashabiki kuanza kuondoka kwa kuhofia usalama wao.
  Katika mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkali, Simba walitangulia kupata dakika ya tisa tu kupitia kwa Nahodha wake, mshambuliaji John Raphael Bocco aliyefunga kwa penalti baada ya mchezaji wa Al Masry, Mohamed Koffi kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
  Bao hilo halikudumu sana, kwani Ahmed Goma aliisawazishia Al Masry inayofundishwa na gwiji wa Misri, Hossam Hassan dakika ya 11  kwa shuti lililomshinda kipa Aishi Manula.
  Al Masry wakapata bao la pili dakika ya 26 kupitia kwa Ahmed Abdalraof ‘Shokry’ aliyefunga kwa penalti baada ya beki Mghana, James Kotei kuunawa mpira kwenye boksi.
  Kipindi cha pili, kocha Mfaransa wa Simba SC, Pierre Lechantre aliwatoa Bocco, beki Yussuf Mlipili na nafasi zao kuchukuliwa na mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo na kiungo Said Ndemla waliokwenda kuongeza nguvu kikosini.
  Kasi ya mchezo wa Simba iliongezeka baada ya mabadiliko hayo na wakafanikiwa kupata bao la pili kufuatia Koffi kuunawa mpira kwenye boksi Mganda, Emmanuel Okwi akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 73.
  Kikosi cha Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, James Kotei, Yusufu Mlipili/Said Ndemla dk71, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco/Laudit Mavugo dk61.
  Al Masry; Ahdem Abdelwahab, Ahmed Abdalraof, Mohamed Mahmoud, Ahmed Gomaa, Islam Salem, Amir Mousa, Islam Atta/Aristide Bance dk81, Mohamed Emam/Issouf Outtara dk81, Farid Emam, Mohamed Koffi na Mohamed Ahmed.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAKATAA UTEJA NYUMBANI, YALAZIMISHA SARE SARE 2-2 NA AL MASRY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top