• HABARI MPYA

    Sunday, March 11, 2018

    PIGO AZAM FC, YAKUBU MOHAMMED NJE WIKI SITA, ZAYED MCHEZAJI BORA WA MWEZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI kisiki wa kati wa Azam FC, Yakubu Mohammed, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa wiki sita kuanzia sasa baada ya kufungwa plasta gumu ‘P.O.P’ kwenye mguu wake wa kulia.
    Yakubu amefungwa P.O.P baada ya kuvunjika mfupa wa nyuma kwenye kifundo cha mguu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya KMC ambao Azam FC ilishinda mabao 3-1 na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
    Daktari wa Azam FC, Dk. Mwanandi Mwankemwa, amesema kuwa beki huyo atakaa na plasta hilo gumu kwa muda wa wiki nne kabla ya kwenda kutolewa.
    Yakubu Mohammed (kulia) atakuwa nje kwa wiki sita kuanzia sasa baada ya kufungwa P.o.P mguu wa kulia

    “Kwa muda wa wiki nne atakuwa na P.O.P na baada ya hapo atakapotolewa P.O.P ataanza programu ya kurejesha mwili kwenye hali ya kawaida (rehabilitation) kwa muda wa wiki mbili kwa hiyo kuanzia sasa kwa muda wa wiki sita hatutakuwa na Yakubu Mohammed,” alisema.
    Akizungumzia majeraha aliyopata jana mshambuliaji wa Azam FC, Mbaraka Yusuph, wakati timu hiyo ikiichapa Mwadui bao 1-0, daktari huyo bingwa wa tiba za michezo alisema wamempumzisha mchezaji huyo kabla ya kumuangalia hali yake kesho.
    “Mbaraka Yusuph jana alipata matatizo ya kugongwa katika msuli wa paja na ni maumivu na leo tumeendelea kumuangalia na kumpumzisha lakini kesho (Jumamosi) tutajaribisha tena kumuangalia yupo katika hatua gani ya maumivu na kuanza mazoezi mepesi mepesi,” alisema.
    Yusuph alishindwa kuendelea na mchezo huo dakika ya 24 tu baada ya majeraha hayo na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Shaaban Idd.
    Wakati huo huo: mshambuliaji Yahya Zayed, ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Januari-Februari.
    Zayd ametwaa tuzo hiyo akiwazidi wachezaji wenzake Nahodha Msaidizi Agrey Moris na kiungo Salmin Hoza, baada ya mashabiki kumpigia kura 102 kati ya 144 zilizopigwa sawa na asilimia 70.8 huku Moris akipata 27 (18.8%) na Hoza 15 (10.4%).
    Mshambuliaji huyo anakuwa mchezaji watano kutwaa tuzo hiyo tokea ianzishwe msimu huu, ikidhaminiwa na wadhamini wakuu wa Azam FC, Benki ya NMB, wengine waliotangulia wakiwa ni Yakubu Mohammed (Agosti), Mbaraka Yusuph (Septemba-Oktoba), Himid Mao (Oktoba-Novemba), Razak Abalora (Desemba-Januari).
    Aidha hiyo ni tuzo ya pili Zayed kuchukua msimu huu, tuzo ya kwanza akichukua kupitia timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) baada ya kuwa Mchezaji Bora wa timu hiyo (Uhai Player Of The Month) mwezi Desemba-Januari.
    Katika hatua nyingine; beki kisiki wa kati wa timu ya vijana ya Azam FC aliyepandishwa kikosi cha wakubwa, Oscar Masai, amefanikiwa kuwa mchezaji bora kwa upande wa timu ya vijana (Uhai Player Of The Month) Januari-Februari baada ya kuwa na mchango mkubwa kwenye timu hiyo.
    Wengine waliotwaa tuzo hiyo inayodhaminiwa na wadhamini namba mbili wa Azam FC, maji safi ya Uhai Drinking water, kwa upande wa Azam B kabla ya Masai ni pamoja na kiungo Twaha Rajab (Agosti) na washambuliaji Paul Peter (Septemba-Oktoba), Andrew Simchimba (Oktoba-Novemba), Yahya Zayd (Desemba-Januari).
    Tuzo za washindi wote zinatarajia kutolewa kesho Jumapili kabla ya mchezo wa Azam FC dhidi ya Mbao, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PIGO AZAM FC, YAKUBU MOHAMMED NJE WIKI SITA, ZAYED MCHEZAJI BORA WA MWEZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top