• HABARI MPYA

    Wednesday, March 07, 2018

    MAYANGA AWAITA WAANDISHI KESHO KUZUNGUMZIA MECHI ZA STARS DHIDI YA ALGERIA NA DRC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga kesho Saa 4:00 asubuhi anatarajiwa kuzungumza na Waandishi wa Habari za Michezo makao makuu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam.
    Pamoja na mambo mengine kocha Mayanga pia atazungumzia kuhusu michezo ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Algeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Taifa Stars inatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki iliyo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwezi huu, ikianzia ugenini nchini Algeria Machi 22 dhidi ya wenyeji, The Greens kabla ya kurejea nyumbani, Dar es Salaam kuwakaribisha The Leopards Machi 27 Uwanja wa Taifa.
    Salum Mayanga (kulia) akifurahi na rafiki zake wa kigeni hivi karibuni Dar es Salaam
    Mara ya mwisho Taifa Stars iliteremka uwanjani Novemba 1 na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa dakika ya 33 kwa penalti na mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Nahodha, Stephane Sessegnon anayechezea klabu ya Montpellier ya Ufaransa.
    Hata hivyo, ilikuwa ni penalti ya mashaka, kwani mchezaji aliyeugusa mpira huo kwa mkono alikuwa ni wa Benin, Khaled Adenon lakini refa akadhani ni mchezaji wa Tanzania.
    Sessegnon akamtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula kufunga bao lake la 21 timu ya taifa katika mechi ya 68.
    Wachezaji wa Tanzania wakamlalamikia refa kwa kutowapa penalti dakika ya 32 kufuatia, winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi baada ya kusukumwa.
    Kipindi cha pili, Tanzania ilikianza kwa nguvu na kasi zaidi wakishambulia kutokea pembeni na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.
    Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Simba ya Tanzania na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri aliyefunga bao hilo akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto dakika ya 50.
    Matokeo haya yanamaanisha Benin ilishindwa kulipa kisasi kwa Tanzania, kwani mara ya mwisho, zilipokutana Oktoba 12, mwaka 2014 Taifa Stars ilishinda 4-1, mabao ya Nahodha wa wakati huo, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16, kiungo Amri Kiemba dakika ya 39, Thomas Ulimwengu dakika ya 49 na Juma Luizio, wakati la Benin lilifungwa na Suanon Fadel dakika ya 90.
    Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 146 kwenye viwango vya FIFA, wakati DRC ni ya 39 na Algeria ni ya 60.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYANGA AWAITA WAANDISHI KESHO KUZUNGUMZIA MECHI ZA STARS DHIDI YA ALGERIA NA DRC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top