• HABARI MPYA

    Sunday, March 04, 2018

    MASHABIKI WAJITOKEZE KWA WINGI TAIFA JUMANNE NA JUMATANO KUZISAPOTI SIMBA NA YANGA

    MECHI mfululizo za michuano ya klabu Afrika zitafanyika Jumanne na Jumatano Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, vigogo wote Simba na Yanga wakicheza.
    Yanga SC ndiyo watakaoanza kuikaribisha Township Rollers ya Botswana Jumanne katika Ligi ya Mabingwa na Simba SC watafuatia Jumatano kuialika El Masry ya Misri katika Kombe la Shirikisho, mechi zote zikiwa ni za kwanza za Raundi ya Kwanza.
    Hiyo ni baada ya timu hizo za Kariakoo, Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam zinazotumia Uwanja wa Manispaa ya Temeke kuwatoa wapinzani wao katika Raundi ya Awali ya michuano hiyo.
    Simba SC iliitoa Gendarmerie Tnare ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-0 ikishinda 4-0 Dar es Salaam na 1-0 Djibouti City, wakati Yanga iliifunga 1-0 Saint Louis Suns United Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda kulazimisha sare ya 1-1 ugenini na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla 2-1.
    Zote, Simba na Yanga katika Raundi hii ya Kwanza zitakutana na wapinzani madhubuti, El Masry ikitoka kuitoa Green Bufalloes ya Zambia kwa jumla ya mabao 5-2, ikishinda 4-0 Cairo na kufungwa 2-1 Lusaka, wakati Township baada ya kushinda 3-0 Gaborone, ikaenda kufungwa 2-1 na El Merreikh ya Sudan mjini Sudan hivyo kuingia Raundi ya Kwanza kwa ushindi wa jumla wa 4-2.
    Kwa namna yoyote huwezi kuzifananisha Gendarmerie na Saint Louis na wapinzani wa wapinzani wa timu zetu katika Raundi ya Awali, Green Buffaloes na El Merreikh – wazi Simba na Yanga zilikutana na timu dhaifu awali.
    Simba na Yanga zinapaswa kujua zinaingia kwenye mechi ngumu za kuwania kusogea mbele kwenye michuano ya Afrika mbele ya wapinzani waliozitoa timu nzuri katika Raundi ya Awali. 
    Tumezishuhudia timu zetu zikicheza mechi mbili mbili zote tangu zizitoe Gendarmerie Tnare na Saint Loius na hazina mabadiliko sana kutoka zilivyokuwa.
    Simba imeendelea kuonyesha ni timu yenye safu nzuri ya ushambuliaji, ikivuna mabao manane katika mechi mbili katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Mbao FC na sare ya 3-3 na Stand United – wakati Yanga imeendelea kuwa timu ya ushindi mwembamba, ikishinda 2-1 mara zote dhidi ya Maji Maji mjini Songea na Ndanda FC mjini Mtwara.
    Hatutarajii mabadiliko sana katika mechi za katikati ya wiki za michuano ya Afrika zaidi ya timu zote mbili kuongeza umakini katika utumiaji wa nafasi, hususan Yanga ambao wanatengeneza nafasi nyingi lakini wanatumia chache.     
    Kitu kikubwa na cha muhimu kinachohitajika katika mechi zote ni mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa Jumanne na Jumatano kuzisapoti timu hizo.
    Wachezaji wa timu zetu hawapaswi kuwa wanyonge Jumanne na Jumatano kwa kucheza huku eneo kubwa la Uwanja wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 likiwa wazi.
    Ni muhimu mno mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumanne na Jumatano kwenda kuzishangilia timu za nyumbani ili kuwatia hamasa wachezaji waweze kucheza kwa juhudi kupigania ushindi.
    Sisi wa soka tunaamini shabiki ni mchezaji wa 12, hivyo kama nguvu ya mashabiki itakosekana tutambue wazi tutazidhoofisha timu zetu katika michezo yake, huku tukijua fika zinakabiliwa na mitihani migumu.
    Pamoja na kuziombea dua zetu katika mechi zake zifanye vyema, lakini tunapaswa kujitokeza kwa wingi siku zote, Jumanne na Jumatano Uwanja wa Taifa kuzishangilia ili ziweze kuzitia nguvu zicheze kwa bidii na kushinda.    Asanteni. Mungu zibariki Simba na Yanga. Mungu ibariki Tanzania. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MASHABIKI WAJITOKEZE KWA WINGI TAIFA JUMANNE NA JUMATANO KUZISAPOTI SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top