• HABARI MPYA

  Sunday, March 04, 2018

  KUZIONA YANGA NA WABOTSWANA SH 5,000 TU JUMANNE TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Yanga na Township Rollers ya Botswana Jumanne kitakuwa ni Sh. 5,000.
  Taarifa ya Yanga leo imesema kwamba viingilio vingine vitakuwa ni Sh. 20,000 kwa VIP A na Sh. 15,000 kwa VIP B na C.  
  Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 10:30 na timu hizo zitarudiana siku 10 baadaye nchini Botswana.
  Township Rollers wamewasili leo mjini Dar es Salaam na kufikia katika hoteli ya Southern Sun katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
  Yanga wapo kambini mjini Dar es Salaam wakiendelea na matayarisho ya mwisho mwisho kuelekea mchezo huo.
  Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikitoka kushinda mechi mbili mfululizo za mashindano ya nyumbani, zote 2-1 ugenini dhidi ya Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma na Ndanda FC mjini Mtwara.
  Hiyo ni baada ya sare ya 1-1 na Saint Louis Suns United katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Mahe, wakitoka kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1.
  Township wenyewe baada ya kuitoa El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda 3-0 Botswana na kufungwa 2-1 Khartoum, walicheza mechi moja tu ya Ligi ya kwao wakifungwa 3-1 na BDF, mabao yote akifunga Mtanzania, Rashid Mandawa.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KUZIONA YANGA NA WABOTSWANA SH 5,000 TU JUMANNE TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top