• HABARI MPYA

    Wednesday, March 07, 2018

    KIPIGO CHA YANGA JANA CHAFICHUA; WACHEZAJI HAWAJALIPWA MISHAHARA MIEZI MITATU, MAKOCHA NUSU MWAKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam wameuanza mwezi wa nne bila kulipwa mishahara, imefahamika.
    Habari za kiuchunguzi ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata ni kwamba mara ya mwisho wachezaji wa klabu hiyo walilipwa mishahara mwezi Novemba mwaka 2017.
    Imeelezwa hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa morali ya wachezaji kushuka na ndiyo maana wengi wao wanaonekana kucheza chini ya viwango vyao kwa sasa.
    Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga alisema kwamba suala la mishahara ni siri baina ya mwajiri na mwajiriwa. “Mishahara ya mchezaji na ofisi ni vitu binafsi, siwezi nikavisemea hivyo. Sisi siyo taasisi peke yake ambayo haijalipa watu mishahara, taasisi zipo nyingi mpaka wakati mwingine serikalini,”alisema.
    Wachezaji wa Yanga (kulia) wakiingia uwanjani jana kwa mchezo na Township Rollers (kushoto)

    Mkwasa amesema hata Waandishi wa Habari pia kwenye vyombo mbalimbali vya Habari nao hawajalipwa zaidi ya miezi sita na Habari haziandikwi, akasistiza masuala ya klabu na waajiri wake yaachwe kuwa siri. 
    Hali ni mbaya ndani ya Yanga kwa ujumla, kwani hata benchi la Ufundi pia, kuanzia Kocha Mkuu George Lwandamina na Wasaidizi wake wote, Mzambia mwenzake Noel Mwandila, wazawa Nsajigwa Shadrack, Juma Pondamali kocha wa makipa, Mohammed Omar ‘Mpogolo’ mtunza vifaa, Jacob Onyango mchua misuli, Meneja Hafidh Saleh na Daktari Edward Bavu nao hawajalipwa kwa zaidi ya nusu mwaka.
    “Hapa maisha ni magumu mno, na mbaya zaidi viongozi kabisa wale wa timu sijui Mwenyekiti (Clement Sanga) na wasaidizi wake hatuwaoni. Sana tunakuwa na Nyika. Wale tunawaolalamikia (Sekretarieti na Makocha) wao nao hali ndiyo mbaya zaidi,” amesema mmoja wa wachezaji, jina tunalifadhi.
    “Yaani watu hapa wanaenda kwa kudra za Mungu tu, kila mtu akili yake haipo kabisa kazini, hakuna morali kabisa. Ni kocha tu ajaribu kutumia busara zake angalau tunaingia uwanjani kucheza,”ameongeza.
    Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiwasalimia wachezaji wa Yanga kabla ya mechi

    Taarifa hizi zinakuja siku moja tu baada ya Yanga SC kufungwa mabao 2-1 na Township Rollers ya Botswana jana katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Pacifique Ndabihawenimana aliyesaidiwa na Willy Habimana na Pascal Ndimunzigo wote wa Burundi, mabao ya Rollers yalifungwa na Lemponye Tshireletso dakika ya 10 kwa shuti la umbali wa mita 20 na Motsholetsi Sikele dakika ya 83, wakati la Yanga lilifungwa na mshambuliji wake Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 30.
    Sasa Yanga inatakiwa kwenda kushinda 2-0 ugenini siku 10 zijazo ili kuingia hatua ya makundi, vinginevyo itaangukia kwenye kapu la kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.  
    Juhudi za kumpata Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga kuzungumzia zaidi kuhusu hali ya klabu hazikufanikiwa kutokana na kutopatikana katika simu yake.  
    Lakini haieleweki kwa nini Yanga inashindwa kulipa mishahara wakati ina wadhamini wakuu wawili, kampuni ya SportPesa na Macron huku pia ikipata fedha kutoka Azam TV na Vodacom za udhamini wa Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPIGO CHA YANGA JANA CHAFICHUA; WACHEZAJI HAWAJALIPWA MISHAHARA MIEZI MITATU, MAKOCHA NUSU MWAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top