• HABARI MPYA

  Thursday, March 15, 2018

  KAMATI YA MAADILI YA TFF YAMFUNGIA MAISHA WAMBURA KUTOJIHUSISHA NA SOKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia maisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu.
  Taarifa ya TFF leo imesema kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
  Hiyo ni baada ya kikao chake cha jana ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
  Wambura amefikishwa kwenye kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
  Akizungumzia hatua hiyo, Wambura amesema kwamba Kamati iliyomfungia haina mamlaka, kwa sababu yeye anawajibika kwenye Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu.
  Wambura amesema kwamba kwa sasa anasubiri barua rasmi kutoka kwenye Kamati hiyo ili kuchukua hatua rasmi. 
  Michael Wambura (kushoto) akiwa na Rais wake, Wallace Karia hivi karibuni

  Wambura amesema mara baada ya kufungiwa kwamba kamati hiyo haina mamlaka ya kufanya, hivyo anawajibika kwenye kamati ya utendaji na Mkutano Mkuu.
  Alisema anasubiri barua rasmi ili kutoa maamuzi juu ya kusimamishwa huko.
  "Kwa sasa sijapata taarifa kamili ya kufungiwa, nikipata barua nitaeleza hatua nitakayofanya," alisema. 
  Wambura alisema suala la kujilipa fedha kupitia, JECK SYSTEM LIMITED ni suala la muda mrefu sana na lipo chini ya TAKUKURU.
  "Hili jambo hilo limepangwa kimikakati na sio suala la kisheria, kwani hapo kuna mambo matatu, ajira za TFF, Fedha na Makamu,"alisema.
  Wambura alisema katika suala la ajira ni baada ya kuleta hoja juu ya nafasi ya katibu mkuu kuhutaji wa kuajiriwa.
  "Ukiangalia nafasi ya Katibu anatakiwa kutangaza pia, haruhusiwi kupewa kama yupo moja ya kamati ya utendaji, kama ilivyo  wa sasa anacheo katika Chama cha makocha, " alisema. 
  Wambura alisema suala la fedha ni baada ya kuwa katika nafasi ya uenyekiti ya kamati ya fedha,  akibaini mambo mengi juu ya matumizi.
  "Ukiangalia matumizi ya miezi sita ni billioni 3 na hakuna tulichokifanya," alisema.
  Alisema kwa hali hiyo atapambana na hizo njama kuhakikishia hatashindwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMATI YA MAADILI YA TFF YAMFUNGIA MAISHA WAMBURA KUTOJIHUSISHA NA SOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top