• HABARI MPYA

  Friday, March 16, 2018

  AZAM FC YAPANIA KUING'OA MTIBWA SUGAR ROBO FAINALI ASFC...YAANZA MAANDALIZI MAPEMAA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche ameahidi mchezo mzuri na ushindi katika mchezo wa Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Machi 31, mwaka huu.
  Kuelekea mchezo huo utakaoanza Saa 1:00 usiku, tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi tangu juzi jioni ili kuhakikisha wanashinda na kwenda Nusu ya ASFC.
  “Mashabiki waendelee kutusapoti kwa sababu mchezo wa mpira unahitaji sapoti, mchezo wa mpira una wachezaji, una viongozi, una mashabiki na mashabiki ndio wanaoongeza chachu ambayo inakuja kufanya mchezo uwe pendwa duniani.
  “Kwa hiyo mashabiki waje kwa wingi watusapoti na sisi tutahakikisha tunawapa furaha ile ambayo wanaitarajia, watarajie mchezo mzuri na wenye ushindi,” alisema Cheche.
  Cheche aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) kabla ya desemba mwaka juzi kupewa nafasi hiyo timu kubwa, alisema mchezo huo utakuwa ni tofauti sana na ule waliocheza kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu na kutoka sare ya bao 1-1.
  “Mchezo wa ligi ni tofauti na FA, huu ni mchezo wa mtoano (knockout) lazima mmoja afungwe kama mnatoka sare mnafika kwenye hatua ya penalti lakini sisi tunataka kuhakikisha mchezo tunaumaliza ndani ya dakika 90 lakini kikubwa mno kwanza ni kuanza kuwajenga wachezaji wetu mazoezini kwa sababu mazoezi ndiyo yatatupelekea kufanya vizuri huu mchezo kwa hiyo tuko makini kuhakikisha watu wanafanya mazoezi vizuri ili mechi iweze kuwa nyepesi kwetu,” alisema.
  Akizungumzia maandalizi waliyoanza, Cheche alisema kuwa kwa sasa watafanyia kazi mazoezini makosa waliyofanya kwenye mechi zilizopita ikiwemo kuwadukua wapinzani wao Mtibwa Sugar.
  “Tunafanyia kazi matatizo tuliyokuwa nayo kidogo kwenye mechi zetu za ligi tulizocheza huko nyuma, kurekebisha makosa, kuangalia kitu gani cha kufanya, kuiangalia Mtibwa uzuri wake na udhaifu wake ili tuandae vijana wetu wahakikishe tunakwenda kuwaangamiza Mtibwa,” alisema.
  Msimu uliopita timu hizo zilikutana kwenye hatua ya 16 bora ya michuano hiyo, mchezo ukifanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 10.00 jioni na Azam FC ikafanikiwa kuibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0, liliwekwa kimiani na Ramadhan Singano ‘Messi’, akiunganisha pasi safi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Mshindi wa mchezo huo, atacheza ugenini kwenye nusu fainali na mshindi wa robo fainali nyingine kati ya Stand United na Njombe Mji, mchezo huo ukipigwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Machi 30 mwaka huu.
  Wakati huo huo: Timu ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 ‘Azam U-20’ imeishushia kipigo kizito cha mabao 15-1 FFU Ukonga, katika mchezo wa kirafiki uliomalizika jioni hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Azam U-20 inayonolewa na Kocha Mkuu Meja Abdul Mingange, ilifanikiwa kupata mabao sita kwenye kipindi cha kwanza, yaliyofungwa na beki wa kulia Abdul Omary ‘Hama Hama’, kiungo Twaha Hashir na Novatus Dismas, kila mmoja akifunga mara mbili.
  Kipindi cha pili Azam U-20 ilijipatia mabao mengine tisa kupitia kwa Richard, Tepsi Evance, Ashraf Said, Said John, Omary Banda, waliofunga moja kila mmoja huku Jamal Abdul na Zackaria Audi wakiingia nyavuni mara mbili kila mmoja.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAPANIA KUING'OA MTIBWA SUGAR ROBO FAINALI ASFC...YAANZA MAANDALIZI MAPEMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top