• HABARI MPYA

    Monday, March 12, 2018

    AZAM FC YAPANDA TENA NAFASI YA PILI LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA MBAO FC 2-1 CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC usiku wa Jumapili imeichapa Mbao FC  mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Licha ya Simba na Yanga kuwa na mechi mbili mkononi kila mmoja, lakini matokeo hayo yanaifanya Azam FC kusogea hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 44 ikiizidi Yanga pointi moja huku ikizidiwa pointi mbili na Simba iliyo kileleni kwa pointi 46.
    Mabao ya Azam FC iliyopata ushindi wa tatu mfululizo, yamefungwa kiustadi na wachezaji waliotokea benchi kipindi cha pili, alianza winga Idd Kipagwile, dakika ya 63 akimalizia kwa kichwa krosi safi ya beki wa kushoto Bruce Kangwa.
    Idd Kipagwile akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Azam FC bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbao FC 
    Kikosi cha Azam FC kilichoanza dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Azam Complex 

    Kipagwile alifunga bao hilo la uongozi sekunde chache mara baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Joseph Mahundi, na kuamsha kelele kwa mamia ya mashabiki wa Azam FC waliohudhuria mchezo huo.
    Dakika tisa baadaye mshambuliaji Bernard Arthur, aliyeingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Shaaban Idd, aliipatia bao la pili Azam FC kwa jitihada binafsi akimalizia pasi safi ya juu ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kabisa hivi sasa.
    Mbao ilijitutumua na kupata bao la kufutia machozi dakika ya 89, lililofungwa na James Msuva, mdogo wa Simon Msuva, winga wa Difaa Hassan El Jadida ya Morocco.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kwa siku nne hadi Alhamisi ijayo kitakapoanza tena maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Mtibwa Sugar Machi 30 mwaka huu.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Mwadini Ali, David Mwantika, Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, Aggrey Moris, Himid Mao, Salum Abubakar 'Sure Boy', Frank Domayo, Shaaban Idd/Bernard Arthur dk61, Yahya Zayed na Joseph Mahundi/Iddi Kipagwile dk63.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAPANDA TENA NAFASI YA PILI LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA MBAO FC 2-1 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top