• HABARI MPYA

  Sunday, February 11, 2018

  YANGA WASIKATE TAMAA, WAFANYIE KAZI MAKOSA WANAWEZA KUFANYA MAAJABU UGENINI

  WACHEZAJI wa timu ya Saint Louis Suns United  ya Shelisheli walikuwa wenye furaha baada ya dakika 90 za mchezo wa jana dhidi ya wenyeji, Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam licha ya kufungwa 1-0.
  Wazi furaha ya St Louis ilitokana na kuwabana wenyeji, hadi wakapata ushindi mwembamba wa 1-0 tu katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Ndiyo, ni ushindi mwembamba uliotokana na bao la kiungo Juma Mahadhi aliye katika msimu wake wa pili Yanga SC tangu asajiliwe kutoka Coastal Union ya Tanga, aliyefunga dakika ya 66 kwa shuti akimalizia kona iliyopigwa na winga Geoffrey Mwashiuya iliyozua kizazaa langoni mwa Saint Louis.
  Mahadhi alifunga bao hilo dakika moja baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib Migomba kama ilivyokuwa kwa mpishi wa bao lake, Mwashiuya ambaye naye alimbadili Emmanuel Martin.
  Na ni bao ambalo lilikuja baada ya zaidi ya saa nzima ya Yanga kusota kujaribu kuupenya ukuta imara wa Saint Louis walioamua kucheza kwa kujihami muda wote ili kujaribu kutoruhusu nyavu zao kuguswa.
  Na Saint Louis wakawa wenye bahati zaidi baada ya Yanga kupoteza hadi nafasi ya kufunga kwa penalti mapema tu kipindi cha kwanza.
  Mshambuliaji Mzambia Obrey Chirwa alipiga nje mkwaju wa penalti dakika ya 25 baada ya beki wa Yanga, Hassan Ramadhani Kessy kuangushwa kwenye boksi na Herve Raktoarison ambaye alionywa kwa kwa kadi ya njano na refa Belay Tedesse Asserese.
  Kwa ujumla, Chirwa mshambuliaji tegemeo Yanga, leo alicheza nyuma ya bahati yake, kwani pamoja na kukosa penalti, alifanya makosa mara kwa mara na kupoteza nafasi zaidi za kufunga.
  Ikafikia Chirwa akapoteza hali ya kujiamini, lakini bado haikutosha kwa kocha Mzambia mwenzake, George Lwandamina kumpumzisha, pengine kutokana na ukweli kwamba hakuwa na mshambuliaji mwingine benchi kwa sababu timu inakabiliwa na maejruhi wengi.
  Pius Charles Buswita, tegemeo lingine la mabao Yanga pamoja na viungo wenzake, Ajib na Martin nao wote hawakuwa kwenye ubora wao leo na haikuwa ajabu walipotolewa kipindi cha pili.
  Nafasi nzuri zaidi ambayo waliipata wageni ni dakika ya 53 wakati Karl Hall kupiga nje akiwa anatazamana na lango la Yanga, baada ya kipa wa kukutana na mpira uliotemwa na kipa, Ramadhan Awa Kabwili.
  Saint Louis walionyesha ni timu inayoweza kushambulia na kufika kwenye eneo la wapinzani – maana yake wanaweza hata kufunga.
  Na baada ya ushindi mwembamba, Yanga watasafiri kwenda Victoria nchini Shelisheli kuyalinda matokeo hayo katika mchezo wa marudiano kati ya Februari 20 na 21, ili kusonga mbele.
  Ukweli ni kwamba matokeo ya jana na namna timu ilivyocheza kwa ujumla inazidi kuwakatisha tamaa wana Yanga juu ya timu yao.
  Ikumbukwe msimu wote huu mashabiki wa Yanga wamekata tamaa na timu yao na wamekuwa hawajitokezi kwa wingi uwanjani inapocheza, wakiaminia hawana kikosi cha hakika cha ushindi kutokana na nyota wao wengi kuwa majeruhi.
  Na Yanga imekuwa ikijikongoja hivyo hivyo msimu huu na pongezi zaidi ni kwa benchi la Ufundi kwa kuweza kuwapa nafasi wachezaji chipukizi, ambao wamekuwa wakijitajidi kuibeba timu pamoja na mapungufu yote.
  Kipa ambaye hajawahi kucheza ligi yoyote ya ushindani, Ramadhani Kabwili anaaminiwa kucheza Ligi Kuu kwanza na sasa anaaminiwa kudaka mechi ya Ligi ya Mabingwa hakika ni mageuzi makubwa ndani ya Yanga.
  Pamoja na yote, matokeo ya jana hayakuwafurahisha wana Yanga na wengi hawana imani kwamba timu inaweza kuvuka raundi hii baada ya mchezo wa marudiano.
  Kwa kweli mashabiki na wapenzi wa Yanga hawapaswi kuikatia tamaa timu yao, bali waendelee kuwa wastahmilifu na wenye subira wakizingatia timu ipo katika kipindi kigumu cha mpito.
  Kwa benchi la Ufundi, baada ya mchezo wa jana bila shaka wameona walikosea wapi. Wameona nguvu ya wapinzani ilipolalia na sasa wanajua namna ya kujipanga kuelekea mchezo wa marudiano.
  Pamoja na yote, Yanga bado ilikuwa timu bora uwanjani jana, ambayo ilinagushwa na makosa na bahati kwa ujumla tuseme.
  Kama Chirwa angefunga penalti yake, Buswita, Ajib, Martin na Kessy wakatumia nafasi nzuri walizopata za kufunga jana leo hadithi ingekuwa nyingine na mashabiki wa Yanga wangekuwa wanatembea vifua mbele.
  Niwakumbushe kitu kimoja wana Yanga; mwaka jana pia timu yao ilishiriki michuano hii na ilianzia ugenini nchini Comoro, ambako mechi ya kwanza Februari 12 ilishinda 5-1 dhidi ya Ngaya Club, lakini mchezo wa marudiano ikalazimishwa sare ya 1-1 Februari; 18 Uwanja wa Taifa.
  Mchezo wa pili ikalazimishwa sare ya 1-1 na Zanaco ya Zambia Machi 11, kabla ya kwenda kutoa sare ya 0-0 pia Machi 18 kwenye mchezo wa marudiano na kutolewa kwa mabao ya ugenini.
  Wazi Yanga inaweza kuibuka na ushindi mnono kwenye mchezo wa marudiano ambao ilistahili kuupata nyumbani kama itajipanga vyema kuelekea mechi hiyo ya wiki mbili zijazo.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WASIKATE TAMAA, WAFANYIE KAZI MAKOSA WANAWEZA KUFANYA MAAJABU UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top