• HABARI MPYA

  Tuesday, February 06, 2018

  YANGA SC WANA SHUGHULI NA NJOMBE MJI FC LEO UWANJA UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DFAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC leo wanateremka Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kumenyana na Njombe Mji FC katika mfululizo wa ligi hiyo.
  Ikiwa ni siku mbili tu tangu wacheze ugenini, Uwanja wa Samora mjini Iringa na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli – Yanga leo wanacheza tena.
  Pamoja na ukweli kwamba wamekuwa na ratiba iliyowabana kucheza mechi mbili ndani ya siku ya nne tena mikoa tofauti, lakini Yanga hawajalalamika na wamejipanga kwa changamoto hiyo.
  Katika mchezo wa leo, Yanga inaweza kuendelea kumkosa kipa wake namba moja, Youthe Rostand ambaye ni majeruhi.
  Rostand alicheza kwa dakika 15 tu Jumamosi mjini Iringa kabla ya kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na kipa wa tatu, chipukizi Ramadhani Awam Kabwili aliyekwenda kumalizia vizuri.
  Ikumbukwe Yanga pia kwa sasa inamkosa kipa wake wa pili, Benno Kakolanya ambaye alikuwa majeruhi, ingawa kwa wiki ya pili sasa taarifa za klabu zinasema amepona. 
  Michezo miwili iliyopita, dhidi ya Ihefu Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) mjini Mbeya na dhidi ya Lipuli, Yanga ilimkosa kiungo wake mshambuliaji mahiri, Ibrahim Ajib Migomba aliyeumia katika mechi dhidi ya Azam FC wiki mbili zilizopita.
  Lakini kwa Yanga ya sasa chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina kumekuwa hakuna mchezaji tegemeo katika timu anaweza kucheza yeyote na timu ikavuna matokeo mazuri.  
  Habari njema zaidi ni kwamba mshambuliaji anayejituma zaidi katika timu, Obrey Chirwa yuko fiti kwa asilimia 100 na leo anatarajiwa kuendelea kuonyesha umuhimu wake katika klabu.
  Mechi zaidi za Ligi Kuu zinatarajiwa kuchezwa kesho; vinara Simba SC wakiwakaribisha Azam FC Uwanja wa Uhuru pia, Mbao FC na Singida United Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Mwadui FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Stand United na Lipuli FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Maji Maji na Tanzania Prisons Uwanja wa Maji Maji Songea na Ndanda FC na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
  Keshokutwa kutakuwa na mchezo mmoja wa Ligi Kuu kati ya  wenyeji, Ruvu Shooting na Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WANA SHUGHULI NA NJOMBE MJI FC LEO UWANJA UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top